Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa leo tarehe 12 Juni, 2026 amezindua majaribio ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma na kuahidi kuwa ndege za abiria kuanza kufanya kutua katika uwanja huo mwezi Julai, 2026.
Akizungumza katika hafla, Mhe. Mbarawa ambaye alikuwa mgeni rasmi ameliagiza Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuharakisha utaratibu wa kuupanga Uwanja wa Ndege Musoma katika ratiba za ndege za abiria ili wananchi wa Mkoa wa Mara waweze kuanza kutumia usafiri huo.
“Ninaiagiza ATCL kuhakikisha kuwa inauingiza Uwanja wa Ndege Musoma katika ratiba za ndege haraka iwezekanavyo ili huduma za usafiri ziweze kutolewa kwa wananchi” amesema Mhe. Mbarawa.
Mhe. Mbarawa amesema majaribio ya utayari katika viwanja vya ndege vya Musoma na Shinyanga yanaashiria kukamilika kwa sehemu muhimu za miradi ya ukarabati na upanuzi wa viwanja hivyo na kuwa tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mhe. Mbarawa amezielekeza taasisi zinazohusika na mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma ambazo ni Wakala wa BArabara (TANROADS) na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (TAA) na wakandarasi kukamilisha sehemu iliyobakia katika mradi huo kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amesema kuzinduliwa kwa majaribio ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma ni maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mara ya mwisho ndege kubwa kutua katika uwanja huu ilikuwa ni Machi, 2018 ambapo ndege ya Precision Air yenye uwezo wa kubeba abiria 45 ilifanya safari yake ya mwisho katika uwanja huu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za kuanza kutumika kwa uwanja huo kuanzisha na kukuza shughuli zao ili kuimarisha uchumi wao kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwenda maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kanali Mtambi amesema kwa sasa wananchi na wafanyabiashara wanauwezo wa kusafiri kwa muda mfupi kufika maeneo mbalimbali jambo ambalo amesema likitumika vizuri linaweza kuchechemua fursa nyingi za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Abdul Mambokaleo amesema kuwa mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja huo ulianza kutekelezwa mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi bilioni 35.
Ndugu Mambokaleo amesema mradi huo pamoja na mambo mengine umeboresha njia ya kuruka ndege kutoka mita 1600 za changarawe yenye uwezo wa ndege za abiria 45 zilizokuwepo hadi mita 1750 za lami zenye uwezo wa kuwezesha ndege za abiria 80 kutua na kuruka katika uwanja huo.
Ndugu Mambokaleo ameahidi kuwa TAA baada ya kulipa fidia kwa wanachi itaanza kujenga kwa kasi jengo la abiria katika uwanja huo na kukamilisha majengo mengine ya kutolea huduma yanayoendelea kukamilishwa katika mradi huo wakati huduma nyingine zinaendelea kutolewa katika uwanja huo.
Hafla ya uzinduzi wa majaribio ya kutua na kuruka kwa ndege Uwanja wa Ndege Musoma imefanyika katika uwanja huo na kuhudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, viongozi na watendaji wa Taasisi za Umma, wabunge wa Mkoa wa Mara, viongozi wa CCM Mkoa wa Mara, viongozi wa dini na wananchi.






Comments
Post a Comment