Serikali imepokea na kuahidi kuifanyia kazi hoja ya kutathmini mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hususan katika majiji yenye uwezo mkubwa wa ukusanyaji wa mapato.
Hoja hiyo iliwasilishwa Bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, ambaye alitaka Serikali kutafakari uwezekano wa kufanya marekebisho ya mfumo huo ili kuzingatia tofauti za mapato kati ya majiji makubwa na halmashauri nyingine nchini.
Dkt. Mahera amesema kuwa wakati halmashauri zote zinatenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya mikopo hiyo, baadhi ya majiji makubwa hukusanya mapato makubwa yanayofanya fedha zinazotengwa kufikia mabilioni ya shilingi.
Ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kuibua haja ya kutafuta uwiano utakaowezesha sehemu ya fedha hizo kuelekezwa pia katika miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara na miundombinu mingine muhimu.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alisema Serikali itaendelea kuboresha sheria na kanuni zinazosimamia mfuko huo kulingana na mahitaji na mazingira ya utekelezaji yanavyobadilika.
Amesema pamoja na majiji makubwa kuwa na mapato makubwa, pia yana idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji huduma za mikopo hiyo, jambo linaloongeza mahitaji ya fedha ikilinganishwa na halmashauri nyingi za wilaya.
Hata hivyo, Dkt. Dugange amesema Serikali imepokea maoni hayo na itafanya tathmini zaidi ili kuona kama kuna haja ya kufanya maboresho yatakayoongeza ufanisi wa mfuko huo huku ukiendelea kutimiza lengo lake la kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Tumepokea hoja hii na tutaendelea kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha zaidi utekelezaji wa mfuko wa asilimia 10,” amesema Dkt. Dugange.

Comments
Post a Comment