MKUU WA JESHI LA MAGEREZA AFUNGUA MAFUNZO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA UREKEBISHAJI KWA MAAFISA USTAWI WA JAMII
Na. Ssgt Mawazo Mtondo - Dodoma.
Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Juni 10, 2026, amefungua rasmi Mafunzo kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kuhusu Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu za Urekebishaji katika Ukumbi wa Rugimbana, Msalato, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, CGP Katungu aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa namna inavyoendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Alisema Serikali imekuwa ikitoa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya magereza, makazi ya watumishi, vyombo vya usafiri pamoja na kugharamia mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa Jeshi la Magereza.
CGP Katungu alibainisha kuwa moja ya majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ni urekebishaji wa wafungwa kwa kuwapatia elimu, ujuzi na maarifa ili wanapomaliza vifungo vyao warejee katika jamii wakiwa raia wema na wenye tija. Alieleza kuwa jukumu hilo limeainishwa katika Sheria ya Magereza, Sura ya 58, Kanuni Na. 62 pamoja na Kanuni za Kudumu za Magereza (Prisons Standing Orders, 2003, 4th Edition), Kanuni Na. 404. Aidha, sheria za kimataifa pamoja na mikataba na matamko mbalimbali ya kikanda vimeendelea kusisitiza umuhimu wa urekebishaji wa wafungwa kwa lengo la kuwajengea ujuzi na maarifa yatakayowasaidia baada ya kumaliza vifungo vyao.
Aliongeza kuwa Mheshimiwa Rais amekuwa akielekeza Jeshi la Magereza kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika eneo la urekebishaji wa wafungwa ili waweze kurejea katika jamii wakiwa na mchango chanya wa maendeleo. Vilevile, Tume ya Kuboresha Mfumo wa Haki Jinai ilitoa mapendekezo mbalimbali yanayolihusu Jeshi la Magereza, ikiwemo kuboresha programu za urekebishaji wa wafungwa. Sambamba na hilo, Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Audit) uliofanywa mwaka 2024 na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (CAG) ulipendekeza kuandaliwa na kutekelezwa kwa Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu za Urekebishaji.
Kutokana na maelekezo na mapendekezo hayo, Jeshi la Magereza limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha utekelezaji wa jukumu la urekebishaji. Miongoni mwa hatua hizo ni kuandaa mitaala mipya ya mafunzo kwa watumishi pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) katika utoaji wa mafunzo kwa wafungwa na watumishi.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Magereza limeandaa Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu za Urekebishaji wa Wafungwa unaobainisha hatua kuu nne za mzunguko wa urekebishaji (Rehabilitation Circle). Hatua hizo ni mapokezi na maelekezo ya awali gerezani (Admission and Orientation), kipindi cha kutumikia kifungo na kupatiwa huduma za urekebishaji (Incarceration Period), maandalizi ya kuachiliwa (Pre-Release) na hatua ya kurejea na kuunganishwa tena katika jamii (Reintegration).
Alisema mwongozo huo utamwezesha kila mfungwa kufanyiwa tathmini ya kina ili kubaini mahitaji yake na kuingizwa katika programu stahiki za urekebishaji. Hadi sasa, makundi yaliyokwisha kupatiwa mafunzo hayo ni Maafisa Mapokezi, Wakuu wa Magereza yote nchini, na sasa wataalamu wa Ustawi wa Jamii, Saikolojia na Sosholojia.
Aidha, CGP Katungu alisema Jeshi la Magereza limeanza kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa vitendo, ambapo utafiti kuhusu urudiaji wa makosa kwa wafungwa waliomaliza vifungo vyao umeanza kufanyika kwa ushirikiano na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki kilichopo Dar es Salaam. Kwa sasa, wataalamu hao wanaendelea na ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya utafiti huo.
Pia, Jeshi la Magereza limeunda timu maalumu ya kuandaa andiko la kuanzisha Mfuko Maalumu wa Kuwasaidia Wafungwa Wanaomaliza Vifungo vyao ili kuwawezesha kujitegemea wanaporejea katika jamii. Vilevile, Jeshi linaendelea kuunda Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wafungwa (PIPMIS) kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA), ambapo utekelezaji wake umefikia hatua nzuri.
Akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Usimamizi wa Wafungwa ya Jeshi la Magereza, SACP Emmanuel Malisa, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Edith Mbogo, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii kuelewa na kutekeleza ipasavyo Mwongozo wa Urekebishaji wa Mwaka 2025. Alibainisha kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa awamu zilizopita na yanakusudia kuimarisha usimamizi wa programu za urekebishaji, kuwajengea washiriki uwezo wa kitaaluma na kuchangia urejeshwaji bora wa wafungwa katika jamii.


























Comments
Post a Comment