Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya CDF CUP 2026 amesema michuano hiyo inatarajiwa kuanza rasmi julai 6 huku lengo likiwa ni kuwaonesha watanzania namna jeshi lao linavyokuza na kuibuq vipaji mbalimbali.
Akizungumza mapema hii leo, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akielezea maandalizi ya michuano hiyo ambapo pia amesema mikakati ya jeshi la Wananchi wa Tanzania ni kuimarisha timu za kijeshi ili kutoa wawakilishi wazuri ndani na nje ya nchi.
Aidha, Brigedia Jenerali Saidi amesema kuwa katika michuano ya mwaka huu jeshi limefanikiwa kufanya maboresho kwa kuja na zawadi za mikanda kwa washindi ikiwa pamoja na kuongeza mchezo wa 'Pool Table' ili kuongeza wigo wa washiriki katika mchezo huwo.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Saidi amesema kuwa miongoni mwa michezo itakayo shindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu, Pool Table, Mchezo wa Mishale, ikiwa pamoja na michezo yote ya mikono.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Benk ya CRDB, Bi. Farida Mbwana ameipongeza kamati ya maandalizi ya michuano hiyo ambapo amesema kuwa michezo ni sehemu ya kujenga jamii ikiwa pamoja na kuimarisha mshikamano wa Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wanamichezo wanzake Mwanariadha mashuhuri kutoka jeshi la Wananchi Alphonce Simbu amempongeza mkuu wa majeshi kwa kufanikisha uwepo wa michuano huku akikiri uwepo wa michezo hiyo husaidia kujiandaa na mashindano ya kimataifa.
Michuano ya CDF Cup 2026 inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano, uzalendo na ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama. Kupitia mashindano hayo, wananchi watapata fursa ya kushiriki na kushuhudia vipaji mbalimbali vya michezo huku wakijenga ukaribu zaidi na jeshi lao.
Mbali na burudani, CDF Cup imeendelea kutambulika kama chombo cha kukuza nidhamu, afya na ari ya kufanya kazi kwa pamoja. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali na hivyo kuimarisha umoja wa kitaifa kupitia michezo.
Wadau wengi wa michezo wanatarajia CDF Cup 2026 kuacha alama kubwa kwa kuibua vipaji vipya na kuimarisha mahusiano kati ya jeshi na jamii. Ujio wa michuano hiyo unaonekana kuwa ishara ya kuendeleza dhana ya kwamba michezo ni daraja muhimu la kuwaleta Watanzania pamoja kwa manufaa ya taifa.







Comments
Post a Comment