WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali imekamilisha majadiliano ya utekelezaji wa Mradi Unganishi wa Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma kupitia mwekezaji mpya wa Kampuni ya Shudao Investment Group Company Limited (SDIG) kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kupitia majadiliano hayo, pande zote zimefikia makubaliano muhimu kuhusu mgawanyo wa hisa, muundo wa uwekezaji, usimamizi wa mradi, kiwango cha mtaji pamoja na uongezaji thamani wa madini ya chuma, vanadium na titanium hapa nchini.
Aidha, rasimu za mikataba ya ubia (JVAs) na wanahisa (SHAs) tayari zimekamilika huku hatua za mwisho za idhini zikiendelea katika mamlaka husika. Serikali inatarajia mikataba hiyo kusainiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 kabla ya kuanza rasmi kwa ujenzi wa mradi utakaotekelezwa kwa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, utekelezaji wa mradi huo utaokoa matumizi ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.22 sawa na Sh trilioni 3.2 ambazo Tanzania imekuwa ikitumia kuagiza bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi.
Pia amesema mradi huo unatarajiwa kuingizia Serikali mapato ya dola za Marekani trilioni 1.99 ndani ya miaka 25 kupitia kodi na mrahaba, sambamba na kuzalisha ajira za moja kwa moja 6,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 26,000.



Comments
Post a Comment