Kwa miezi kadhaa sasa, siasa za Uganda zimeendelea kutikiswa na wimbi la tuhuma, uchunguzi wa kifedha na vita ya chini kwa chini ya kuwania madaraka ndani ya Bunge la taifa hilo, huku jina la Spika Anita Among likiendelea kutawala mijadala ya kisiasa nchini humo.
Among, ambaye kwa muda mrefu alionekana kuwa mmoja wa wanasiasa wenye nguvu kubwa ndani ya utawala wa Rais Yoweri Museveni, sasa anakabiliwa na presha kubwa kisiasa kufuatia tuhuma za ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na uchunguzi unaodaiwa kuwagusa baadhi ya viongozi waandamizi serikalini.
Kupanda kwake kisiasa kulikuwa kwa kasi kubwa. Baada ya kifo cha aliyekuwa Spika Jacob Oulanyah mwaka 2022, Anita Among alichaguliwa kuongoza Bunge na haraka akajijengea ushawishi mkubwa ndani ya chama tawala cha NRM pamoja na miongoni mwa wabunge.
Uwezo wake wa kusimamia mijadala ya Bunge kwa msimamo mkali ulimfanya kuwa mmoja wa watu muhimu zaidi ndani ya mfumo wa utawala wa Museveni.
Lakini nyuma ya nguvu hiyo ya kisiasa, mawimbi ya tuhuma yalianza kuongezeka.
Katika miezi ya karibuni, makundi ya wanaharakati wa kupambana na rushwa pamoja na wapinzani wa serikali wamekuwa wakitaka uchunguzi wa kina kufanyika dhidi ya matumizi ya fedha ndani ya Bunge.
Mijadala kuhusu matumizi ya kifahari ya viongozi, mali zinazodaiwa kuongezeka kwa kasi pamoja na madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma ilianza kutawala vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini Uganda.
Presha iliongezeka zaidi baada ya baadhi ya mataifa ya Magharibi kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya viongozi wa Uganda wanaotuhumiwa kuhusishwa na rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu akiwemo Spika Among
Hatua hizo ziliongeza taharuki ndani ya serikali huku wachambuzi wakisema taswira ya viongozi wakuu wa Uganda imeanza kupata doa kimataifa.
Kadri hali ilivyoendelea kuwa ngumu, taarifa kutoka ndani ya duru za kisiasa mjini Kampala zilianza kueleza kuwa Anita Among ameanza kupoteza uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya makundi yenye ushawishi ndani ya chama tawala.
Ripoti hizo zimedai kuwa viongozi kadhaa wa NRM wameanza kufanya vikao vya siri kujadili mustakabali wa uongozi wa Bunge na uwezekano wa kupata Spika mpya.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kisiasa, hali hiyo ndiyo iliyosababisha kuanza kwa mchakato wa chini kwa chini wa kutafuta mrithi wa Among.
Majina ya baadhi ya mawaziri akiwemo Waziri wa ulinzi Dokta Oboth Oboth, wabunge waandamizi pamoja na viongozi wenye ukaribu na Ikulu yamekuwa yakitajwa kuwania nafasi hiyo nyeti.
Ndani ya NRM, makundi mbalimbali yanaonekana kupimana nguvu huku kila upande ukitaka kuhakikisha mtu wao anapata nafasi ya kuongoza Bunge ambalo ni mhimili muhimu wa kisiasa nchini humo.
Katika hatua iliyozua mjadala mkubwa, taarifa rasmi zinaeleza kuwa Anita Among mwenyewe amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuendelea kuwania nafasi ya Spika ili kupunguza presha dhidi yake na kulinda umoja wa chama tawala.
Wachambuzi wanaamini kuwa hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya makubaliano ya kisiasa ya ndani ya NRM ili kuzuia mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Ingawa hakuna tamko rasmi lililotolewa na Among kuhusu kujiondoa kwake, baadhi ya wabunge wa karibu naye wameanza kutoa kauli zinazodokeza kuwa anaweza kutafuta nafasi nyingine ya kisiasa au kubaki ndani ya mfumo wa serikali bila kuendelea kuwania uspika.
Mchakato wa kumpata Spika mpya unatajwa kuwa wa tahadhari kubwa kutokana na umuhimu wa nafasi hiyo katika kusimamia shughuli za Bunge na kuhakikisha serikali inapita salama katika mijadala mikubwa ya kisiasa na sheria.
Kwa muda mrefu, nafasi ya Spika imekuwa ikitajwa kuwa moja ya nafasi zenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Uganda baada ya urais.
Kwa sasa, macho ya wengi yanaelekezwa Kampala huku vita ya chini kwa chini ya urithi wa Anita Among ikiendelea kushika kasi. Swali kubwa linalobaki ni nani ataibuka kuwa sura mpya ya kuongoza Bunge la Uganda katika kipindi hiki kigumu cha kisiasa.


Comments
Post a Comment