![]() |
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali imepanga kuanzisha Kitengo cha Intelijensia ya Masoko na Viwanda kwa lengo la kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Akizungumza leo Mei 22, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Kapinga amesema hatua hiyo inalenga kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za masoko, teknolojia na fursa za biashara duniani.
“Katika mazingira ya sasa ya ushindani wa biashara na viwanda duniani, taarifa sahihi za masoko na teknolojia ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara,” amesema Kapinga.
Amesema Serikali imebaini changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa taarifa za masoko ya kimataifa, mahitaji ya bidhaa katika misimu tofauti, viwango vya ubora pamoja na vikwazo vya kibiashara.
“Kumekuwapo changamoto ya kutokujua bidhaa zinazohitajika katika misimu mbalimbali, viwango vya ubora na vikwazo vya kibiashara,” amesema.
Aidha, Waziri huyo amesema kitengo hicho kitakuwa na jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa za masoko ya kimataifa, kubaini fursa za biashara, kutoa tahadhari za mabadiliko ya masoko pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara kupata taarifa muhimu kwa wakati.
Amesema kuanzishwa kwa kitengo hicho ni hatua muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea taarifa sahihi, ushindani na teknolojia za kisasa.

Comments
Post a Comment