Kikundi Cha amani chataka kasi iongezwe kukamata wanaotukana mitandaoni

GEORGE MARATO TV
0


...Yapongeza siku 100 za Rais madarakani

MASHAKA MHANDO, Tanga

KIKUNDI cha Amani nchini kimeitaka Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi, kuongeza kasi ya kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali watu wanaojiita wanaharakati wa mitandaoni wanaotumia majukwaa hayo kupotosha ukweli na kuichafua Serikali.

Kauli hiyo imetolewa jijini Tanga katika mkutano maalum wa kikundi hicho uliolenga kuhamasisha uzalendo, kuelezea mafanikio ya Serikali na kupongeza utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais tangu alipochaguliwa 2025.

Akisoma risala ya kikundi hicho, Mjumbe wa Kikundi cha Amani, Rehema Manyama, alisema katika kipindi cha siku 100, Rais ameonyesha dira na uthubutu wa hali ya juu kwa kufanikisha utoaji wa Bima ya Afya kwa wote, kuzalisha ajira kwa vijana 12,000, kutoa mikopo, na kuituliza nchi dhidi ya misukosuko ya kisiasa.



"Rais wetu ameonyesha dira ya kweli. Ndani ya siku 100 ameweza kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kutoa fursa za kiuchumi. Tunashauri ngazi za mikoa ziendelee kutoa elimu ya uzalendo na kuimarisha elimu ya amali ili vijana wajiajiri na kuingiza kipato," alisema Manyama.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Amani nchini, Hassan Hamisi Kubebelwa, aliwaasa wananchi, hususan vijana, kuacha kushawishiwa na watu wanaoshinda kwenye mitandao ya kijamii wakielezea mabaya pekee na kuficha mazuri mengi yanayofanywa na Serikali.

"Lengo la kuja Tanga ni kuwahamasisha wanakikundi wenzetu wasimame kidete kuelezea maendeleo ya miundombinu mkoani hapa na nchi nzima. Tuache kusikiliza upotoshaji wa mitandaoni; Serikali imaleta fedha za mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri, watu wakope na kujiendeleza badala ya kulalamika," alisisitiza Kubebelwa.

Naye Mjumbe Zuberi Gogo, alibainisha kuwa ingawa hitilafu ndogo ndogo haziwezi kukosekana, changamoto kubwa inatokana na baadhi ya watendaji wanaopindisha taratibu na kuigombanisha Serikali na wananchi. Alitoa wito kwa wananchi kuelewa taratibu za kiserikali ili wasipotezwe na upotoshaji.

Akizungumzia suala la mikopo, Mjumbe Zainabu Salim Ugata, alifafanua kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri haina upendeleo, bali inatolewa kwa vikundi vilivyofuata taratibu zote zilizowekwa. Alisema kikundi hicho kitaendelea kuzunguka mikoa yote nchini kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa mambo ya Serikali.

Washiriki wa mkutano huo waliazimia kuwa ni wajibu wa kila mzalendo kuilinda taswira ya nchi na kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi zinazotolewa na Rais zinawafikia walengwa bila vikwazo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top