Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imetangaza kufuta vyama vyote vya siasa na kuhamisha mali zao zote kuwa mali ya serikali, kufuatia amri iliyopitishwa na mamlaka za nchi hiyo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana tarehe 29 Januari mjini Ouagadougou, katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Kiongozi wa Taifa hilo, Kapteni Ibrahim Traoré.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Émile Zerbo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuijenga upya dola, akieleza kuwa mfumo wa vyama vingi uliokuwepo awali ulikuwa na matatizo makubwa, ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na kukosa ufanisi.
Kwa mujibu wake, tathmini ya serikali imebaini kuwa kuongezeka kwa idadi ya vyama vya siasa kulichochea migawanyiko ndani ya jamii na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa.
Kabla ya mapinduzi ya mwaka 2022, Burkina Faso ilikuwa na zaidi ya vyama 100 vya siasa vilivyosajiliwa, huku 15 kati yao vikishikilia viti katika Bunge baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Msemaji wa serikali, Pingdwendé Gilbert Ouédraogo, amesema ripoti kadhaa zilifanyiwa mapitio kabla ya uamuzi huo kuidhinishwa rasmi.
Aidha, muswada tofauti unaobatilisha sheria zilizokuwa zinasimamia uendeshaji wa vyama vya siasa, ufadhili wa vyama pamoja na hadhi ya kiongozi wa upinzani pia umepitishwa, na unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Mpito.
Kwa mujibu wa amri hiyo, vyama vyote vya kisiasa vinafutwa rasmi na mali zao zitachukuliwa na serikali. Mamlaka zimesema hatua hiyo inalenga kulinda umoja wa taifa na kusaidia mageuzi ya kisiasa katika kipindi cha mpito.

Comments
Post a Comment