Katika siku zake Mia moja za mwanzo madarakani Ikiwa Wananchi wa Tanzania watampatia ridhaa ya kuongoza tena serikali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan, amebainisha kuwa atafanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya afya nchini, ikiwa ni pamoja na kugharamia kwa asilimia mia moja vipimo na matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa saratani, figo, moyo, Sukari, mifupa na mishipa ya fahamu.
Aidha katika kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote, ndani ya Siku mia moja za mwanzo ikiwa atashinda uchaguzi Mkuu, Rais Samia pia ameahidi kuzindua rasmi mfumo wa taifa wa bima ya afya kwa wote kwa awamu ya majaribio kwa kuanza na wazee, watoto, wajawazito pamoja na watu wenye ulemavu, akisema gharama za matibabu kwa makundi hayo ya jamii zitabebwa na mfuko wa Taifa wa bima ya afya kwa wote.
Wakati akiainisha vipaumbele vyake ndani ya siku mia moja ikiwa ataibuka mshindi katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Rais Samia kwenye hotuba yake mbele ya wananchi waliokusanyika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers Jijini Dar Es Salaam, ameahidi pia kuajiri wahudumu wapya wa afya 5,000 ikiwemo wakunga na wauguzi kama sehemu ya mpango wake wa kuendelea kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto.
“Aidha tutapiga marufuku hospitali yoyote nchini kuzuia miili ya marehemu kuchukuliwa na ndugu zao hata jamaa gharama za matibabu hazijalipwa. Tutakuja na mfumo mwingine wa kuhakikisha jamaa wa marehemu wanalipa gharama lakini sio kuzuia miili ya watu waliotangulia mbele za haki.” Ameongeza Rais Samia.
Rais Samia pamoja na Mgombea mwenza wake Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi na Mgombea Urais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi wameanza rasmi safari zao za kujinadi na kueleza mipango na sera walizonazo kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, ambapo Rais Samia amewaomba wananchi kujitokeza pia kwa wingi kwenye Mikutano yao ya hadhara ili kufahamy sera na mipango waliyonayo kuelekea mwaka 2030 ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi ya kuwachagua Viongozi bora kwa maendeleo ya miaka mitano ijayo.























