Na Shomari Binda-Musoma
WAZAZI na walimu wa shule ya msingi Bukoba B wamemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma mjini kwa kuwachangia magunia mawili ya mahindi ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Shukrani hizo wamezitoa leo mei 9,2025 kwenye kikao cha wazazi kilichofanyika shuleni hapo wakati wa kujadili maendeleo ya shule hiyo.
Wakizungumza baada ya mbunge huyo kuzungumza kwa njia ya simu kwenye kikao hicho kutoka bungeni jijini Dodoma wamesema moyo wa upendo alionao katika kusaidia masuala ya kijamii unapaswa kushukuliwa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo James Makanya licha ya kumshukuru mbunge huyo amesema mtoto anapopata chakula shuleni walau mlo mmoja unamuongezea uwezo wa kufatilia masomo darasani.
Amesema suala la chakula lina umuhimu mkubwa na kuwaomba wazazi kumuunga mkono mbunge kwa kuhakikisha wanachangia chakula na kuwa suala endelevu.
Makanya amesema chakula ambacho wazazi watakichangia kwaajili ya wanafunzi kitatumika kwa malengo kusudiwa.
" Tunamshukuru sana mbunge kwa moyo wake na kutambua umuhimu wa chakula kwa wanafunzi na kuamua kuchangia gunia 2 za mahindi.
"Wazazi ni ombi kwenu kuhakikisha suala la kuchangia linakuwa endelevu ili wanafunzi wapate walau mlo mmoja wakiwa hapa shuleni",amesema.
Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Marco Lukaijakale amewaeleza wazazi umuhimu wa wanafunzi kupata chakula shuleni na kudai utaratibu wa kuchangia utawekwa vizuri na kuwa rafiki.
Kwa upande wake afisa lishe shuleni hapo Albin Mathias amesema wanafunzi wanapokaa muda mrefu shuleni pasipo kupata chakula ni vigumu kupata uelewa mzuri wanapofundishwa.
Nao wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi Bukoba B wamesema wapo tayari kuchangia chakula ili watoto wapate kujifunza vizuri.





