Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi Millioni Mia Saba kwenye utoaji wa Mikopo ya Asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Taasisi hiyo imeokoa shilingi Millioni 706.2 kutokana na Uhakiki na Udhibiti uliofanyiia kwenye utoaji wa Mikopo ya Vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Protas Henry amesema kuwa katika Uhakiki huo,Vikundi 41 ambavyo Mikopo yake ilikuwa na Thamani ya Millioni Mia Saba havikukidhi vigezo.
Vikundi hivyo vilibainika kuwa na Makosa mbalimbali ikiwemo Kuomba mkopo hewa,kuwasilisha kwa kamati vielelezo vya kughushi mfano Profoma invoice na kuwasilisha Mikataba ya uongo ya maeneo ya kufanyia biashara,kuwasilisha bei za Juu za vifaa kuliko bei ya soko,kutokuwa na maeneo ya kufanyia biashara pamoja na Kuomba mkopo kwa ajili ya mradi wa mtu binafsi au familia.
"TAKUKURU imechukua hatua ya kufanya Udhibiti wa kuziba mianya ya Rushwa iliyojitokeza ili kusaidia Halmashauri kutoa Mikopo kwa Vikundi vilivyokidhi vigezo" Alisema Henry katika Taarifa yake kwa umma na kuongeza kuwa
"Vikundi 87 vilikidhi vigezo kati ya vikundi 128 vilivyoomba Mikopo ambapo Jumla ya shilingi Billioni 1.3 vilitolewa kwa vikundi hivyo"
TAKUKURU Mwanza pia imeokoa shilingi Millioni 17.3 na kuziwasilisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Fedha hizo ni malipo ya Kodi ya Zuio kutokana na Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Elimu iliyofuatiliwa na Taasisi hiyo katika kipindi cha kuanzia Januari Hadi Machi Mwaka huu.
Katika kipindi hicho,TAKUKURU imefuatilia Miradi 23 ya Maendeleo yenye Thamani ya shilingi Billioni 11.3 ambapo Miradi 20 yenye Thamani ya Billioni 9.1 imebainika kuwa na mapungufu kadhaa na kutoa mapendekezo ya namna Bora ya kuboresha Miradi hiyo.
Aidha TAKUKURU Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza imeokoa shilingi Millioni 64 ambazo ni malipo ya wachimbaji wadogo wa madini kutoka kwa Mwekezaji wa Kampuni ya LHT Mining Co. Ltd
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mwanza Protas Henry amesema kuwa Mwekezaji huyo aliingia Mkataba na kikundi cha Nyabayombe kinachomiliki eneo la mgodi lililopo kijiji cha Nyabayombe wilayani Misungwi ili kuwalipa fidia ya kuwaondoa wamiliki wa maduara katika eneo hilo.
"Hata hivyo, Kampuni ya LHT Co.Ltd ilivunja wa Makubaliano baina yake na Kikundi cha Nyabayombe bila kufuata Taratibu za Mkataba ikiwemi kutohusishwa kwa wanakikundi na hivyo kusababisha wamiliki wa maduara kutopata stahiki zao.Alieleza Henry na kuongeza kuwa
" Uchunguzi wa Kina wa TAKUKURU umeokoa kiasi hicho cha shilingi Millioni 64 ambacho kimesaidia wamiliki hao wa maduara kulipwa stahiki zao,Aidha uchunguzi zaidi unaendelea na iwapo itabainika kuwepo kwa Makosa ya Jinai wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria"
Pamoja na mafanikio hayo,katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025,upande wa uchunguzi na mashtaka,Taarifa 88 zilipokelewa ambapo 68 zinahusu Rushwa huku 20 zikiwa hazihusu Rushwa,Uchunguzi kuhusu Taarifa zinazohusu Rushwa umeanzishwa na ziko katika hatua mbalimbali za Uchunguzi.
TAKUKURU kupitia programu yake ya Rafiki imefanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa matundu 19 ya vyoo katika shule ya msingi Saba Saba iliyoko wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Ujenzi wa vyoo hivyo ulichukua muda mrefu bila kukamilika kwake,hali ambavyo ingeweza kusababisha kutokea kwa Vitendo vya Rushwa Mathalani fedha kuchepushwa na Mradi kutokamilika kwa Kiwango kilichokusudiwa.











