Na Angela Sebastian; Bukoba
Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera imeokoa zaidi ya shilingi milioni 52.6 kwa kipindi cha miezi mitatu ambazo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali sambamba na za wananchi waliokuwa wametapeliwa fedha kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali jana mjini Bukoba katika ofisi za taasisi hiyo kaimu mkuu wa Takukuru mkoa Hajinas Onesphory alisema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu Takukuru, walifanikiwa kurejesha vigae vyenye thamani ya shl.mil 50,368,000 kutoka kwa mzabuni aliyepewa kazi ya kujenga hospitali ya Wilaya ya Missenyi.
"Katika ufuatiliaji huo tulibaini kutokuwepo na kutotumika vigae vya zaidi ya thamani ya mil 50.3 ambavyo vilinunuliwa na Serikali ambapo havikuwasilishwa kwenye mradi huku nyaraka zote za mapokezi na manunuzi zikionyesha kuwepo na kupokelewa kwenye mradi"alisema Onesphory
Alisema baada ya kubaini hilo Takukuru walifuatilia kwa kina kwa kimshirikisha mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi vigae hivyo vinarejeshwa na kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo na hatua dhidi ya mtuhumiwa zitachukuliwa pindi uchunguzi utakapokamilika.
Wakati huo huo kupitia dawati la uchunguzi la Takukuru wamefanikiwa kusaidia wananchi tisa wa kijiji cha Bulembo kata Ibuga Wilayani Muleba waliokuwa wamedhulumiwa kwa kuchangishwa fedha jumla ya shl mil.2,300,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa wakala wa umeme vijijini (REA) unaotekekezwa na kampuni ya Nakuroi Investment Ltd Wilayani humo.
"Kijiji hicho hakikiwemo katika mpango wa kufikishiwa umeme kwa wakati huo hivyo,mafundi hao waliwalaghai wananchi watoe fedha hizo ili wapelekewe umeme huku wakijua wazi kuwa jambo hilo haliwezekani,baada ya kupata taatifa hiyo tulifanya uchunguzi na kuwafikisha mahakama watuhumiwa wawili"alieleza Onesphory
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Patric Method na Revocatus Masanja ambapo walifikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Muleba kwa makosa ya Rushwa chini ya kifungu cha 15 cha kupambana na rushwa ambapo baada ya kesi hiyo kusikilizwa mbele ya hakimu Daniel Nyamkyelya walitiwa hatiani kwa makosa ya udanganyifu na mahakama iliwaamuru fedha zote mil shl 2.3 zirejeshwe na zilizochukuliwa na watuhuliwa.
Fedha hizi zimekabidhiwa kwa wananchi hao tisa na taasisi hiyo na watuhumiwa wamechukuliwa hatua ya kufukuzwa kazi na mwajiri wao ambaye ni kampuni ya Nakuroi.
Mmoja wa wananchi waliorejeshewa fedha zao Akwilina Philemoni alithibitisha Takukuru kwa kuwezesha fedha hivyo kurejeshwa huku akiwashauri waendelee kuwasaidia na wengine ambao wanatapeliwa ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

.jpg)


