Halmashauri ya wilaya Bariadi Mkoani Simiyu imekabidhi Majengo yaliyokuwa ya shule ya Sekondari Tarajali ya wasichana Matongo kwa wizara ya maliasili na Utalii ili yatumike kufundishia Taaluma ya wanyamapori.Makabidhiano ya Majengo hayo,Mkuu wa wilaya Bariadi Simon Simalenga amesema kuwa uwepo wa Chuo cha Taaluma ya Uhifadhi wa maliasili katika wilaya ya Bariadi kutatoa fursa kwa jamii kujifunza pamoja na kutumia mbinu za kuzuia wanyama wakali na waharibifu ikiwemo Tembo.

Simalenga aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa Simiyu kwenye hafla hiyo amesema kuwa kuwepo kwa chuo cha Taaluma ya wanyamapori wilayani Bariadi pia kunatarajia kufungua fursa nyingi zikiwemo za kiuchumi na hivyo kuchochea ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya uhifadhi wa wanyamapori
Kwa Mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya Bariadi,Moja ya Mipango ya Mkoa Simiyu ni kujenga uwanja wa Ndege ambao utatumika kuleta watalii wa Nje na ndani ili kuendeleza azma ya serikali ya kuufungua zaidi Mkoa huo.
Shule hiyo yenye Jumla ya majengo Tisa imekabidhiwa kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula Septemba 12 mwaka huu kwa ajili ya kutumika kuendesha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi watakaokuwa wanasoma kozi za usimamizi wa wanyamapori na waongoza watalii katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.
Uamuzi wa kukabidhi Majengo hayo ambayo awali yalikusudiwa kutumika kama sekondari ya wasichana umekuja kufuatia kutotimia kwa dhamira hiyo kutokana na kujengwa katika eneo linalokabiliwa na changamoto ya uvamizi wa tembo
Katika kuepusha athari hiyo kwa wanafunzi wa kike na kufuatia pia kujengwa kwa shule mpya ya wasichana katika wilaya ya Bariadi,serikali ya mkoa wa Simiyu ilifikia maamuzi ya kutoa majengo ya shule tarajali ya wasichana Matongo kwa wizara ya maliasili na utalii ili yatumike kama taasisi ya kutoa mafunzo ya uhifadhi wa maliasili nchini.
Katika hotuba yake,Naibu Waziri Kitandula amesema kuwa kutumika kwa eneo hilo lililopo kata ya Giliya kuendeshea mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma kwenye Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutatoa fursa ya kiulinzi katika eneo husika na maeneo inayopakana nayo.
Kitandula amesema kuwa hatua hiyo inawahakikishia ulinzi wananchi waliokuwa wanavamiwa na wanyama wakali na waharibifu mara kwa mara na wakati mwingine wanyama hao kusababisha vifo.
Naibu Waziri Kitandula ametumia hafla hiyo kuwakumbusha wataalam wa halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuanzisha shughuli za kijamii kwenye maeneo ya mapito ya wanyama (shoroba) au karibu na hifadhi za taifa au mapori ya akiba.
Kitandula amesisitiza kuwa ni lazima wakati wote uanzishwaji wa shughuli za maendeleo uzingatie mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Shule ya sekondari ya Wasichana Matongo ilianza kujengwa tangu enzi za serikali ya awamu ya nne.
Shule hiyo pamoja na kukamilika haikuwahi kudahili wanafunzi kutokana na kuwepo kwa changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo ambao mara kwa mara wamekuwa wakivamia eneo husika na kusababisha madhara kwa wakazi wa maeneo hayo na wakati mwingine kusababisha vifo.