Serikali imekamilisha ujenzi wa Taasisi ya uhasibu Tanzania(TIA)kampasi ya Nyang'homango mkoani mwanza ili kusogeza huduma ya elimu kwa wananchi wa kanda ya ziwa
Waziri wa fedha Dkt.Mwigulu Nchemba amekagua ujenzi wa Taasisi hiyo na kueleza kuridhishwa na matumizi ya shilingi billioni 7.3 zilizotumika kugharamia ujenzi huo.
Nchemba amesema kuwa uwepo wa Taasisi hiyo utachochea ongezeko la shughuli za kiuchumi katika eneo la Nyang'omango na kata ya usagara kwa ujumla na kuwaasa wananchi kutumia fursa ya chuo hicho kubuni miradi ya kujikwamua kiuchumi.
Waziri Nchemba amesema kuwa ujenzi wa Taasisi hiyo ni mkakati wa serikali wa kujenga miundombinu bora ya elimu ili kuimarisha mazingira ya kujifunza na kufundishia.
"Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuwaletea watanzania maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu ambayo imegusa nyanja zote ikiwemo elimu na afya,hakuna eneo lolote nchi hii ambayo haijanufaika na miradi mathalani ya elimu"alisema Nchemba
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Palangyo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Taasisi hiyo imepokea shilingi billioni 58.1 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika kampasi zake nane.
Profesa Palangyo amesema kuwa maboresho ya miundombinu yamewezesha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kutoka 12,870 mwaka 2016/2017 hadi kufikia 28,979 mwaka 2023/2024.
Ongezeko la udahili wa wanafunzi limewezesha Taasisi ya uhasibu Tanzania kuongeza mapato pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Kampasi ya TIA mwanza ilianzishwa mwaka 2012 katika Jengo la kupanga ikiwa na wanafunzi 1,792,idadi ambayo imeongezeka hadi kufikia 1,980 baada ya kujengwa kwa kampasi Maya katika eneo la Nyang'omango yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,430 kwa wakati mmoja.
Awali Waziri Nchemba amekutana na uongozi wa wilaya misungwi ambapo Mkuu wa wilaya hiyo Johari Samizi amemueleza kuwa wilaya hiyo imepokea shilingi billioni 39 ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha miaka iliyopita.
Akizungumza na viongozi hao,Nchemba amewataka kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao ili kuwezesha miradi kutekelezwa kwa ubora na kwa thamani halisi ya fedha.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa amani mjini misungwi,waziri wa fedha amewahakikisha wananchi kuwa serikali itatatua kero zinazowakabili ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji ya Ukiriguru-Usagara-Sumve, Ilujamate-Buhingo pamoja na Idetemya.