Na Robinson Wangaso – Mwanza.
Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania THRDC kanda ya Ziwa, umesema matukio ya utekwaji na kuibiwa kwa watoto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa mwaka 2023/2024 yakiwemo matukio ya mauaji ya watu wenye Ualibino yaliyoripotiwa ni 73 jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hstua na kudhibitiwa kwa namna ya pekee ili kukomesha matukio hayo.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 26, 2024 jijini Mwanza, katika tamko la pamoja lililotolewa na mashirika 55 yanayojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu kutoka mikoa ya kanda ya ziwa Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga baada ya kumalizika kwa mafunzo na mkutano mkuu wa Mwaka wa kanda, ulifanyika katika hotel ya Gold Crest kwa kwa uratibu na ufadhiliwa na THRDC.
Tamko hilo limesomwa kwa niaba ya wenzake na Edwin Soko, mwanachama wa mtandao huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari za kupiga vita dawa za kulevya na uharifu nchini Tanzania.
Soko ameainisha kuwa matukio hayo yakiwemo ya watoto 33 walitekwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, matukio 20 ya mauaji na kutekwa watu wenye Ualbino. Tamko hilo limebainisha kuwa katika matukio hayo baadhi ya wahanga waliuawa na kujeruhiwa kisha kuondolewa kwa baadhi ya viuongo vya miili ya wahanga hao.
‘’Tunasisitiza na kuiomba serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto, watu wenye Ualibino na makundi mbalimbali hasa wakati huu wa kuelekea katika chaguzi za serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025’’ alisema Edwin Soko akiwa anasoma tamko la watetezi wa haki za Binadamu kanda ya Ziwa.
Watetezi hao wa haki za Binadamu kupitia tamko hilo la kulaani mauaji, utekaji na matukio ya kupotea kwa watoto nchini, wametoa rai kwa mamlaka mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya waziri mkuu, kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyia mwakanin 2025.
Katika hatua nyingine, mtandao huo umemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume huru kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekwaji wa watu, ili ichunguze tuhuma za matukio ya hayo ambayo baadhi yake yameripotiwa na kutuhumu baadhi ya vyombo vya dola kuwa vinahusika na matukio hayo.
Tamko hilo limetaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni Mathias Dida Songoma ambaye alikatwa mkono wa kulia na kupelekea kifo chake katika kijiji cha Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Tukio lingine lile la kujeruhiwa kwa Happines Raphael, Mwanafunzi wa chuo kikuu cha mtakatifu Agustino mkoani Mwanza aliyekuwa anasoma mwaka wa kwanza ambaye alishambuliwa kwa kujeruhiwa kwa panga na watu wasiojulikana muda wa saa 3 usiku katika eneo la Malimbe tukio lililofanyika Desemba 31, 2023.


Comments
Post a Comment