Mbunge wa Jimbo la Ilala na Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ameibeba ajenda ya makazi na ustawi wa wananchi kwa kuitaka NHC kujenga nyumba za gharama nafuu zitakazowawezesha wananchi wa kipato cha chini na cha kati kupata makazi bora bila kubanwa na gharama kubwa za upangaji.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi wa Mitaa ya Kibasila na Kitonga, Kata ya Upanga Mashariki, Zungu alisema maendeleo ya miji yanapaswa kwenda sambamba na kulinda maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa uwekezaji wa makazi usiwe chanzo cha kuwaondoa au kuwaumiza wananchi waliotegemea nyumba hizo kwa miaka mingi.
"Tunataka maendeleo yanayowajali wananchi. Nyumba za gharama nafuu zinawezekana na zina hadhi. NHC inapaswa kujenga nyumba zitakazowapa wananchi fursa ya kuishi kwa heshima na usalama," amesema Zungu.
Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya maji, ukosefu wa vivuko salama vya waenda kwa miguu katika maeneo ya shule pamoja na changamoto zinazowakabili wapangaji wa nyumba za NHC.
Akijibu hoja hizo, Zungu ametangaza kuwa Juni 14 atawakutanisha viongozi wa NHC wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu pamoja na Bodi ya Shirika hilo na wapangaji wa Ilala ili kusikiliza malalamiko yao na kupata ufumbuzi wa kudumu.
"Sitaruhusu sauti za wananchi zipuuzwe. NHC itakuja kukutana na wananchi ili kusikiliza kero zao na kujenga mwafaka utakaolinda haki za kila upande," amesema.
Aidha, alieleza kuwa Bunge litaendelea kuangalia namna ya kuimarisha mifumo ya kisheria itakayosaidia kulinda haki za wapangaji na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa haki na uwazi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki, Sultan Salim, alimpongeza Zungu kwa kusimama na wananchi, akibainisha kuwa baadhi ya wapangaji wameishi katika nyumba za NHC kwa zaidi ya miaka 40 huku wakitekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa uaminifu.
"Wananchi hawa wamekuwa sehemu ya maeneo haya kwa miongo kadhaa. Ni muhimu haki zao zikazingatiwa na taratibu zote za kisheria ziheshimiwe," amesema Sultan.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wataalamu kutoka DAWASA, TARURA, NHC pamoja na wadau wa usafi wa mazingira, ambapo wananchi walipata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa mamlaka husika.
Naye Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Ilala, Selina Shodawali, amesema viongozi wa eneo hilo wataendelea kushirikiana kuhakikisha kero zote za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.













Comments
Post a Comment