Mbunge wa Jimbo la Ilala na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amemtaka mkandarasi anayejenga Shule ya Sekondari ya Mfano ya CRDB iliyopo Kata ya Upanga Mashariki jijini Dar es Salaam kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kutumika Januari 2027.
Mhe. Zungu ametoa maelekezo hayo Juni 7, 2026 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo akiwa ameambatana na TullyEsther Mwambapa.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Mhe. Zungu ameipongeza CRDB Bank chini ya uongozi wa Abdulmajid Nsekela kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Amesema mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni tano ni uwekezaji muhimu utakaosaidia kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi.
Kabla ya ukaguzi huo, Mhe. Zungu alishiriki mkutano wa kikanuni wa maendeleo wa wananchi wa Kata ya Upanga Mashariki ulioongozwa na Diwani wa kata hiyo, Sultan Salim, ambapo wananchi walipata fursa ya kuwasilisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.
Mkutano huo wa kikanuni wa maendeleo wa wananchi wa Kata ya Upanga Mashariki uliolenga kusikiliza, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
Mkutano huo uliongozwa na Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki, Sultan Salim, na kufanyika Juni 7, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Upanga, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wananchi, Mhe. Zungu alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kutatua changamoto za maendeleo, huku akiahidi kufuatilia masuala yaliyoibuliwa ili kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa viongozi kukutana na wananchi mara kwa mara ili kusikiliza maoni yao na kuimarisha utoaji wa huduma katika ngazi ya jamii.









Comments
Post a Comment