*Elimu bila malipo, Bima ya Afya kwa Wote ni ushindi*
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa, Stephen Wasira, amesema ujamaa bado ni msingi mkuu unaoendesha sera na mipango ya maendeleo nchini.
Akizungumza na wanachama wa CCM mjini Moshi, leo Juni 6 2026, Wasira alisema alikana madai kuwa mfumo huo umepitwa na wakati.
"Wale wanaojidanganya hawaujui. Misingi inayoendesha nchi sasa ni ileile ya ujamaa. Tuanzie na elimu bila malipo, tuendelee na jitihada za kuanzisha Bima ya Afya kwa wote. Haya yote ni mafanikio ya ujamaa," alisema.
Wasira alitoa mfano wa Mkoa wa Kilimanjaro, akibainisha kuwa kama sio ujamaa, ardhi na mashamba ya kahawa yangekuwa yamenunuliwa na watu binafsi na wananchi wasingeweza kumiliki.
"Kama hapa Kilimanjaro tungekosa ujamaa, kahawa yote ingenunuliwa. Ni uongo kusema ingekuwa bado mikononi mwa wananchi," alieleza.
Pia, alizungumzia umuhimu wa uwekezaji wa sekta binafsi, akisema ni jambo la kawaida na la lazima kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akimnukuu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: "Watu wote hawatakuwa na mapato sawa. Mkulima wa nyanya Kilimanjaro na mchimbaji wa gesi Lindi hawawezi kulingana. Hata wachimbaji madini nao hawalingani na wale wasiochimba."
Kwa mujibu wa Wasira, serikali inaleta haki kwa kuwatoza kodi wenye uwezo na kuwasaidia wasio na uwezo.
"Huwezi kujenga nchi bila mtaji. Wenye mtaji ni watu binafsi na kampuni. Kazi yetu ni kuwatoza kodi na kuwasaidia wanyonge," alisema.














Comments
Post a Comment