KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini, mdau wa maendeleo wa Kata ya Nyamatare, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Bw. Fortinatus Magambo, amewekeza zaidi ya shilingi milioni 125 kugharamia ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Msingi Ring'wani.
Bw. Magambo, ambaye ni mzaliwa wa Kata ya Nyamatare na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), amechukua hatua hiyo baada ya kushuhudia hali duni ya miundombinu ya shule hiyo, ambapo wanafunzi walikuwa wakisomea katika madarasa chakavu yasiyokidhi mazingira bora ya kujifunzia.
Akiamini kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii, aliamua kutumia sehemu ya fedha zake binafsi pamoja na kuhamasisha marafiki zake kuchangia mradi huo, ili kuhakikisha watoto wa Ring'wani wanapata mazingira salama, bora na yanayowapa fursa ya kujifunza kwa ufanisi.
Ujenzi wa madarasa hayo unatarajiwa kuondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa, kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuongeza ari ya walimu katika utoaji wa elimu, huku ukiimarisha juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi, wazazi pamoja na viongozi wa Kata ya Nyamatare, ambao wameeleza kuwa ni mfano wa kuigwa wa uzalendo na moyo wa kujitolea kwa maendeleo ya jamii.
Wamesema mchango wa Bw. Magambo utaacha alama ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kwani utasaidia kuinua kiwango cha elimu, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuwajengea mazingira yanayowawezesha kutimiza ndoto zao.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 125 ni ushahidi kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya elimu na ustawi wa jamii.






Comments
Post a Comment