Wazee wa Mila wa Koo 12 za Wakuria, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wametoa wito kwa vijana nchini kutokubali kutumiwa katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya Taifa, huku wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuendelea na ajenda ya maridhiano kwa kuzingatia ombi la kumwachia huru Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu.
Akizungumza katika kikao Cha wazee wa Mila wa Koo 12 za wakuria, Mzee Morisi Mung'oso, mzee wa Koo ya Butimbaru, amesema kikao chao kilijadili masuala matatu muhimu ambapo walimpongeza Rais Samia na Serikali yake kwa hatua walizochukua katika kudumisha amani na utulivu nchini baada ya matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa mwaka 2025.
Mzee Mung'oso Amesema wazee hao wanaamini amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba Serikali imeonyesha uthabiti katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unalindwa.
Pili, amesema wamekemea kauli za viongozi wanaodaiwa kutumia lugha ya matusi na uchochezi dhidi ya viongozi wa nchi, wakisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuhifadhi mshikamano wa Taifa.
Katika hoja yao ya tatu, Mzee Morisi amesema wazee hao wanamuomba Rais Samia kuendelea na sera ya maridhiano kwa kuzingatia uwezekano wa kumwachia huru Tundu Lissu.
"Kupitia dhana ya maridhiano iliyoanzishwa na Mheshimiwa Rais Samia, tunamuomba afikirie kijana wetu Tundu Lissu ili naye apate nafasi ya kuungana na Watanzania wengine katika kujenga Taifa na kuendeleza amani."
Naye Charles Mwita, wa Koo ya Butimbaru, aliwataka vijana kutokubali kudanganywa na watu wanaowasukuma kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Alisema Tanzania imejengwa katika misingi ya amani na kwamba vijana wanapaswa kuwa walinzi wa urithi huo badala ya kuwa sehemu ya migogoro.
"Vijana wetu wasikubali kudanganywa. Amani ndiyo msingi wa maendeleo. Bila amani hakuna maendeleo, na kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda."
Mzee Charles pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaochochea uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa salama.
Kwa upande wake, Mzee Joseph Mwaricha, wa Koo ya Bumela, alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya Watanzania, wakiwemo wasomi na viongozi, wakitoa kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko badala ya kuhimiza umoja.
Amesisitiza kuwa wazee wa mila wanaamini katika mazungumzo, heshima kwa viongozi na mshikamano wa kitaifa.
"Sisi wana Tarime tunahitaji maendeleo, si vurugu. Bila amani hakuna maendeleo, hivyo vijana wetu waungane kujenga Taifa badala ya kuligawa."
Naye Mzee Mtongoli, wa Koo ya Bukila, amempongeza Rais Samia kwa juhudi za kuleta maendeleo na kudumisha amani nchini, akisema Tanzania imebarikiwa kuwa na utulivu unaopaswa kulindwa na kila mwananchi.
Amewataka vijana kuendelea kuhubiri amani na kukataa vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha machafuko.
"Tanzania ilipata uhuru kwa amani, nasi tuna wajibu wa kuendelea kuilinda amani hiyo. Tuendelee kuhubiri umoja na mshikamano kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo."
Wazee wa Mila wa Koo 12 za Wakuria wamesema lengo lao ni kuona Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani, huku wakiwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika kulinda utulivu, umoja na maendeleo ya Taifa.














Comments
Post a Comment