LAMU, Kenya:
Baada ya kutumikia kifungo cha miaka minne gerezani, mwanamume aitwaye Mwendwa Kilatya alirejea kumtafuta Hakimu Mkazi Eugene Pascal Nabwana, aliyekuwa amemhukumu katika Mahakama ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, ili kumshukuru na kumuomba msaada wa kuendelea na masomo ya chuo kikuu.
Kilatya alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kosa la wizi wa mifugo. Kabla ya hukumu hiyo, alikuwa ameacha shule akiwa Kidato cha Tatu, licha ya kuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri darasani. Akiwa gerezani, aliamua kurejea masomoni na kufaulu kwa matokeo mazuri, jambo lililompa matumaini ya kuendelea na elimu ya juu baada ya kumaliza kifungo chake.
Baada ya kuachiwa huru, Kilatya alisafiri hadi Mahakama ya Wamunyu, Kaunti ya Machakos, ambako Hakimu Nabwana alikuwa amehamishiwa, ili kumshukuru kwa uamuzi wake ambao anasema ulimsaidia kubadili maisha yake na kumwelekeza katika njia sahihi.
Akiguswa na simulizi na juhudi za Kilatya, Hakimu Nabwana aliahidi kuwashirikisha marafiki zake kuchangisha fedha zitakazomwezesha kijana huyo kujiunga na chuo kikuu Septemba Mwaka huu ili kutimiza ndoto yake ya kupata elimu ya juu.

Comments
Post a Comment