SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wanatarajia kufanya sensa ya vyombo vya usafiri wa majini nchini katika hatua inayolenga kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kuboresha usimamizi, usalama na maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Akizungumza leo Jun 3,2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salumu amesema sensa hiyo itasaidia kufanya uhakiki na uboreshaji wa takwimu zilizokusanywa mwaka 2021 ili kuakisi hali halisi ya sasa ya sekta ya usafiri wa majini.
Amesema sensa iliyofanyika mwaka 2021 ilibaini kuwepo kwa takribani vyombo 6,000 vya usafiri wa majini, lakini makadirio ya sasa yanaonyesha idadi hiyo inaweza kuwa imeongezeka hadi kufikia vyombo 21,600. Hivyo, sensa mpya itatoa taswira sahihi ya ukubwa wa sekta na kusaidia kupanga mikakati bora ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Amina Msengwa amesema ushirikiano huo utaimarisha mfumo wa takwimu nchini na kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi zitakazosaidia kupanga na kusimamia maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini kwa ufanisi zaidi.
Ameeleza kuwa takwimu zitakazopatikana kupitia sensa hiyo zitasaidia kuongeza ushindani wa kibiashara, kuvutia uwekezaji na kuweka msingi imara wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu katika sekta hiyo.
Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, akibainisha kuwa matokeo yake yatawanufaisha kupitia kuboreshwa kwa utambuzi wa vyombo, usimamizi wa huduma na utoaji wa huduma bora zaidi kutoka Serikalini.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TASAC, Nashon Sigala amesema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa matumizi ya takwimu za kisasa katika sekta ya usafiri wa majini, hatua itakayochangia kuimarisha usafirishaji majini na kukuza uchumi wa nchi.



Comments
Post a Comment