Tanzania imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya hakimiliki na kulinda ubunifu barani Afrika kupitia ushiriki wake katika mkutano wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Watunzi na Wasanii (CISAC Regional Committee for Africa - CAF) uliofanyika Juni 1 na 2, 2026 mjini Paris, Ufaransa.
Ujumbe wa Tanzania kutoka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), ulioongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki, Bi. Naomi Mungure, ulikutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, na kumweleza kuhusu mafanikio na mijadala iliyofanyika katika mkutano huo.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni maendeleo, fursa na changamoto zinazotokana na matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) katika sekta ya hakimiliki, mifumo ya usajili na uhakiki wa kazi za ubunifu, ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha, pamoja na njia za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za hakimiliki barani Afrika.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, Balozi Yakubu aliwapongeza wajumbe hao kwa kuiwakilisha vyema nchi katika jukwaa hilo muhimu la kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya hakimiliki nchini ili kulinda ubunifu, kuongeza mapato ya wasanii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu.
Aidha, aliahidi ushirikiano wa karibu kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa na taasisi za Tanzania zinazoshiriki katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanaendelea kuwakilishwa ipasavyo na fursa zinazopatikana zinawanufaisha wabunifu na wasanii wa Tanzania.
Ujumbe huo pia uliwajumuisha Mkuu wa Hakimiliki wa Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO), Bi. Maureen Fondo, pamoja na aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Bi. Doreen Sinare. Wataalamu hao walimweleza Balozi kuhusu tafiti zinazoendelea katika eneo la hakimiliki na mchango wake katika kuimarisha ulinzi wa kazi za ubunifu barani Afrika.




Comments
Post a Comment