Serikali imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kutekeleza mradi wa upanuzi wa Barabara ya Tunduma mkoani Songwe, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani zikiwemo Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila, bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ambayo Serikali imeipa kipaumbele kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha biashara za kikanda.
Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya usafiri ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Amefafanua kuwa kufuatia ziara ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, katika eneo la Tunduma, maelekezo yalitolewa ya kuhakikisha changamoto ya msongamano wa magari inapatiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia upanuzi wa barabara hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara ya Ujenzi tayari imemkabidhi kazi mkandarasi wa ndani, NARUMO Construction Company Limited, ambaye ameanza utekelezaji wa mradi huo baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina. Mradi huo umeongeza eneo la upanuzi kutoka mita 700 za awali hadi zaidi ya kilomita moja ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya usafiri katika lango hilo muhimu la biashara.
“Tunduma ni lango muhimu la uchumi wa Tanzania na nchi jirani. Kuboresha barabara hii kutapunguza msongamano, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kuimarisha zaidi biashara za kikanda,” amesema Ulega.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafiri, kuondoa ucheleweshaji wa magari mpakani na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa njia kuu ya biashara kwa mataifa yanayotegemea Bandari ya Dar es Salaam.


Comments
Post a Comment