RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wanafunzi wa elimu ya juu kujiandaa kwa dunia inayohitaji ujuzi zaidi ya vyeti, akisisitiza umuhimu wa maarifa, nidhamu, uzalendo, utu, udadisi na uwezo wa kushirikiana nje ya mipaka ya tamaduni, taaluma na mataifa.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo jijini Moscow baada ya kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University), kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya elimu, ushirikiano wa kimataifa na urafiki kati ya mataifa.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameitambua heshima hiyo kama utambuzi wa nafasi ya elimu katika maendeleo ya jamii na uchumi, pamoja na uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi uliosaidia kujenga kizazi cha wataalamu waliochangia maendeleo ya mataifa hayo mawili.
"Katika dunia inayobadilika kwa kasi, jukumu letu ni kuwaandaa vijana wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuongoza katika uchumi wa maarifa," amesema Rais Samia.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania imeweka elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kiini cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku programu ya ufadhili wa masomo ya Samia Scholarship ikiendelea kupanua fursa za elimu kwa Watanzania vijana wenye uwezo na vipaji katika fani za kimkakati.
Mpango huo, ulioanzishwa mwaka 2023, tayari umenufaisha zaidi ya wanafunzi 5,000 na sasa unaelekezwa katika maeneo ya sayansi ya data, akili unde, tiba, uhandisi, mafuta na gesi, pamoja na teknolojia za mazingira.
Kwa upande wake, Rais wa Chuo, Prof. Vladimir Mikhaylovich Filippov, amesema Shahada ya Heshima aliyotunukiwa Rais Dkt. Samia hutolewa kwa nadra kwa viongozi wanaotoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, urafiki na ushirikiano kati ya mataifa.
"Uamuzi wa Baraza la Chuo ni utambuzi wa mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania na Urusi na kuendeleza urafiki kati ya wananchi wa mataifa yetu," amesema Prof. Filippov.
Ameongeza kuwa, Tanzania ni mmoja wa washirika wakuu wa RUDN barani Afrika, na kwamba uamuzi wa kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Heshima ulipitishwa kwa azimio moja na Baraza la Chuo kupitia kura ya siri iliyofanyika tarehe 16 Machi, 2026.
Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Oleg Yastrebov, alisema Tanzania ina nafasi ya pekee katika historia na ushirikiano wa chuo hicho barani Afrika.
"Ushirikiano kati ya RUDN na vyuo vikuu vya Tanzania unaingia katika hatua mpya yenye fursa kubwa zaidi za elimu, utafiti na ubunifu," amesema Prof. Yastrebov.
Aidha, amesema Watanzania wamekuwa wakisoma RUDN tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1960 na kwamba ushirikiano wa sasa baina ya Tanzania na chuo hicho unaendelea kupanuka kupitia ushirikiano katika tafiti za pamoja na programu za maendeleo ya rasilimali watu.
Kando ya hafla hiyo, Tanzania na Urusi zilisaini mikataba mitatu ya ushirikiano katika elimu ya juu, na programu mbili za pamoja za shahada kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha RUDN katika Sayansi ya Takwimu, Mifumo ya Anga, Akili Unde na "Machine Learning."
Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) kilianzishwa mwaka 1960. Chuo kina zaidi ya wanafunzi 46,000 kutoka nchi zaidi ya 160, na programu zaidi ya 800.
Tanzania na RUDN zina ushirikiano wa zaidi ya miaka 65. Hadi sasa, Watanzania 1,132 wamehitimu RUDN, idadi inayoiweka Tanzania katika nafasi ya pili barani Afrika kwa wingi wa wahitimu wa chuo hicho, ikitanguliwa na nchi ya Nigeria. Kwa sasa Watanzania 72 kati ya 200 wanaoendelea na masomo nchini Urusi, wanasoma Chuo Kikuu cha RUDN.
Viongozi wengine wa Afrika waliowahi kutunukiwa Shahada za Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Peoples' Friendship University of Russia (RUDN) ni pamoja na Hayati Sam Nujoma, Rais wa Jamhuri ya Namibia, aliyetunukiwa mwaka 1998.
Mheshimiwa José Eduardo dos Santos, Rais wa Jamhuri ya Angola, aliyetunukiwa mwaka 1998; Mheshimiwa Thabo Mvuyelwa Mbeki, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, aliyetunukiwa mwaka 1998.
Mheshimiwa Olusegun Obasanjo, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria, aliyetunukiwa mwaka 2001; Mheshimiwa Alpha Condé, Rais wa Jamhuri ya Guinea, aliyetunukiwa mwaka 2016; na Mheshimiwa Hery Rajaonarimampianina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar, aliyetunukiwa mwaka 2018.









Comments
Post a Comment