Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Zacharius Kamonga, amesema Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ndani ya jimbo hilo, hali iliyosaidia kuboresha maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Kamonga amebainisha mafanikio na changamoto zilizopo katika sekta za elimu, maji, umeme na barabara, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo vijijini.
Katika Sekta ya Elimu Kamonga amesema sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa kupitia ujenzi wa shule mpya za sekondari pamoja na taasisi za mafunzo ya ufundi.
Amezitaja baadhi ya shule mpya kuwa ni Rubonde, Mkia, Ugera, Ruhuhu na Chifldasta Masasi, akisema shule hizo zimeongeza fursa kwa watoto wa Ludewa kupata elimu karibu na makazi yao.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa pamoja na Baadhi ya vyuo umeongeza fursa kwa vijana kupata mafunzo ya vitendo na ujuzi wa kujiajiri ambapo amesema pia bado kuna changamoto katika elimu ya msingi.
“Shule nyingi za msingi bado zina changamoto ya miundombinu kama vyoo, madarasa na mazingira ya kujifunzia. Hili linahitaji kipaumbele zaidi,” amesema.
Poa sekta ya maji, Kamonga amesema wananchi wa Ludewa bado wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama.
Amesisitiza kuwa maji ni haki ya msingi ya binadamu na Serikali inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ili kupunguza changamoto hiyo.
Katika sekta ya umeme vijijini, Mbunge huyo ameipongeza Serikali kwa kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vingi vya Ludewa, hatua ambayo amesema imeleta mabadiliko makubwa kiuchumi.
Hata hivyo, amesema bado kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa kikamilifu na hivyo yanahitaji kuunganishwa na gridi ya taifa.
Kadhalika Katika Miundombinu ya Barabara Ametoa wito kwa Mamlaka husika Kutumia teknolojia bora ,Akizungumzia miundombinu ya barabara za vijijini, Kamonga amesema Serikali imefanya kazi kubwa, lakini changamoto ya uharibifu wa barabara kutokana na maji bado ni kubwa.
Amesema kuna umuhimu wa kutumia teknolojia bora zaidi za ujenzi pamoja na kuimarisha mifereji ya maji ili barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuhimili magari ya mizigo.
Ameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za maendeleo katika sekta zote muhimu, huku akisisitiza ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi na maendeleo yanaendelea kusonga mbele katika Jimbo la Ludewa.


Comments
Post a Comment