MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wakazi wa Kambi ya Samaria iliyopo Hombolo kulinda na kutunza miundombinu ya huduma za kijamii iliyojengwa kupitia mradi wenye thamani ya shilingi milioni 69.9, ili iweze kudumu na kuendelea kuwanufaisha kwa miaka mingi ijayo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi miradi ya maji, umeme na majiko banifu iliyotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhe. Senyamule alisema jukumu la kutunza miundombinu hiyo sasa liko mikononi mwa wanufaika.
"Miradi hii imewekwa na inahitaji kutunzwa. Tumeshawekewa umeme, kazi ya kutunza balbu ni yetu, si ya REA tena. Tumewekewa maji karibu na makazi yetu, kazi ya kutunza koki ni yetu, si ya STAMICO tena. Ilindeni na kuitunza miundombinu yote mlioletewa kwa sababu thamani yetu ni kuitunza," alisema.
Aidha, aliwahimiza wakazi wa kambi hiyo kutumia huduma hizo kujiongezea kipato kupitia shughuli za uzalishaji, hususan kilimo cha umwagiliaji, ili kuongeza usalama wa chakula na kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Yusuph Ismail alisema mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha makundi yenye mahitaji maalumu yanapata huduma muhimu zinazoboresha maisha yao na kuchochea maendeleo jumuishi.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bi. Zainab Mabuye, alisema uongozi wa Wilaya utaratibu shughuli za kilimo cha umwagiliaji, hususan mboga mboga, ili kuongeza kipato cha wakazi wa kambi hiyo na kuboresha mazingira.
Mradi huo ulianza kutekelezwa baada ya tathmini iliyofanyika Desemba 2025. Umehusisha kufunga umeme katika nyumba 29, kuweka mfumo wa umeme kwenye miundombinu ya maji, kujenga mnara wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 20,000, kutandaza mabomba ya maji yenye urefu wa kilomita 1.55, kujenga vyoo vya kisasa pamoja na kugawa majiko banifu. Jumla ya gharama za utekelezaji wa mradi huo ni shilingi milioni 69.9.
Kambi ya Samaria Hombolo ilianzishwa mwaka 1984 kwa ajili ya kuwahifadhi wazee na watu wenye ulemavu wa viungo uliotokana na ugonjwa wa ukoma waliokuwa wametengwa na familia zao. Baadaye, Mchungaji wa kanisa Anglikana, Canon John Ntandu, kwa msaada wa wadau kutoka Ireland, alijenga nyumba 35 za kudumu kwa ajili








Comments
Post a Comment