MKUU wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka wazazi na walezi nchini kuweka kipaumbele katika malezi ya watoto kwa kuzingatia maadili, mila na desturi za Kitanzania, akisisitiza kuwa familia ndiyo msingi wa kujenga kizazi chenye nidhamu, uzalendo na uwezo wa kuliletea taifa maendeleo endelevu.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Njombe, Mhe. Mtaka amesema wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye upendo, nidhamu na maadili mema yatakayowawezesha kukua wakiwa raia wema, wenye kuwajibika na kuheshimu sheria za nchi.
Amesema malezi bora hayaishii katika kuwapatia watoto mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi, makazi na elimu, bali yanapaswa kuambatana na kuwafundisha heshima, uwajibikaji, uzalendo, uadilifu, uchapakazi na kuheshimu utu wa wengine ili waweze kuwa nguzo ya maendeleo ya jamii na taifa.
"Mtoto mwenye malezi bora anakuwa mwananchi mwema na kiongozi bora wa kesho. Ni jukumu la kila mzazi na mlezi kuhakikisha watoto wanakua katika misingi ya maadili ya Kitanzania badala ya kuathiriwa na mienendo isiyofaa inayoweza kuwapotosha," amesisitiza Mhe. Mtaka.
Aidha, amewatahadharisha wazazi na walezi dhidi ya kuwaachia watoto uhuru usio na mipaka au kuiga mifumo ya malezi isiyozingatia utamaduni na maadili ya Kitanzania, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mmomonyoko wa maadili na kuongeza changamoto za kijamii zinazoweza kuathiri mustakabali wa taifa.
Mhe. Mtaka amesema malezi ya mtoto si jukumu la wazazi pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima, ikiwa ni pamoja na walimu, viongozi wa dini, viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla. Amesema ushirikiano huo utasaidia kujenga kizazi chenye maadili, kinachoheshimu sheria, kuthamini kazi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Magoda, ambapo alipata fursa ya kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kukamilishwa kwa wakati ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Baadaye alihitimisha ziara yake katika Shule ya Msingi Lunyanywi, ambako alipokea taarifa kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu na kutoa maelekezo mbalimbali yaliyolenga kuongeza ubora wa miundombinu ya shule pamoja na kuboresha huduma za elimu kwa manufaa ya wanafunzi na jamii.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Serikali wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa, pamoja na kuimarisha huduma za elimu ili kuendelea kuwajengea watoto wa Kitanzania mazingira bora ya kujifunzia na kufikia ndoto zao.




Comments
Post a Comment