JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limewakamata watuhumiwa 200 wanaodaiwa kufanya makosa mbalimbali ya jinai, huku wengine 51 wakihukumiwa vifungo gerezani, wakiwemo watatu waliohukumiwa miaka 30 kwa makosa ya kulawiti, kuzini na maharimu, na kusafirisha dawa za kulevya.
Akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari mkoani humo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni na doria zilizofanyika kuanzia Juni Mosi hadi Julai 16, mwaka huu.
Kamanda Mchunguzi amebainisha kuwa, licha ya matukio hayo, hali ya usalama mkoani Tanga ni shwari na Jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kupitia falsafa ya Polisi Jamii.
Akifafanua kuhusu watuhumiwa 51 waliohukumiwa baada ya upelelezi kukamilika, Kamanda Mchunguzi amewataja waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kuwa ni Julius Mustafa aliyepatikana na hatia ya kulawiti, Kilimo Issaya aliyepatikana na hatia ya kuzini na maharimu, na Sadiki Waziri aliyepatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.
"Watuhumiwa wengine walipata vifungo vya miaka mitano gerezani kwa makosa ya wizi wa mifugo na jinai nyinginezo ikiwemo kubaka, kujeruhi, kutishia kuua na kuingia nchini bila kibali," amesema ACP Mchunguzi.
Kuhusu watuhumiwa 200 waliokamatwa katika msako huo, Kamanda huyo ameeleza kuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya unyang'anyi, wizi, kuharibu miundombinu, kumiliki noti bandia na kupatikana na nyara za Serikali.
Katika hatua nyingine, ACP Mchunguzi amesema Jeshi hilo limeendeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambapo watuhumiwa 29 walinaswa. Kati yao, watu 14 walipatikana na bunda 750 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 45, na wengine 15 walikamatwa na misokoto na kete za bangi.
Pia, watu watano walikamatwa na nyara za Serikali na mali za wanyamapori, huku pikipiki 20 zisizo na namba za usajili zikikamatwa.
Kamanda Mchunguzi ameongeza kuwa katika operesheni hizo wamefanikiwa kukamata mali mbalimbali za wizi pamoja na vifaa vya miundombinu ya TANESCO na barabara vilivyokuwa vimehujumiwa. Mali nyingine zilizokamatwa ni noti bandia za fedha za Kenya, televisheni 10, na simu za mkononi 25.
Akizungumzia hali ya usalama barabarani, Kamanda Mchunguzi amesema madereva 10,028 wamekamatwa kwa kukiuka sheria za usalama barabarani, huku madereva tisa wakifungiwa leseni zao za udereva kutokana na makosa makubwa likiwemo la mwendokasi.
Amemalizia kwa kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa za viashiria vya uhalifu kwa Jeshi la Polisi ili kudumisha amani na usalama mkoani humo.








Comments
Post a Comment