Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi, wamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimkakati kwa kusaini makubaliano yatakayoongeza kasi ya maendeleo katika sekta za biashara na uwekezaji, kilimo, uchukuzi, afya, elimu na nishati. Makubaliano ambayo yanatarajiwa kuimarisha uchumi wa mataifa yote mawili na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi na mgeni wake aliyekuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja nchini, Rais Samia amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Misri tayari umezaa matokeo makubwa, ikiwemo kuwapatia huduma za upasuaji wa kwa wagonjwa wa moyo wa kitanzania wapatao 420 pamoja na utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye thamani ya takribani shilingi trilioni 7.4.
Rais Samia pia amesema viongozi hao wamekubaliana kuendeleza maboresho ya Bandari ya Bagamoyo kwa kuiunganisha na mtandao wa reli hadi bandari ya Kwala ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo huku pia ikifungua fursa mpya kwa kqtika sekta ya anga kupitia Shirika la Ndege la Air Tanzania kwa kuongeza safari kati ya Tanzania na Misri, hatua inayotarajiwa kukuza biashara, utalii na uwekezaji.
Ameeleza kuwa makubaliano hayo pia yanatoa kipaumbele katika kuvutia uwekezaji wa pamoja, kubadilishana teknolojia na utaalamu pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, hatua hiyo itaongeza ushindani wa uchumi wa mataifa hayo na kuchochea ajira, uzalishaji na biashara ndani ya Bara la Afrika.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Tanzania na Misri zimekubaliana kupanua ushirikiano katika sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kubaini fursa mpya za kiuchumi zitakazochangia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji na kujenga uchumi endelevu kwa manufaa ya mataifa hayo na Bara la Afrika kwa ujumla.
Kwa upande wake, Rais Abdel Fattah El-Sisi amesema lengo la ziara yake ni kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Misri, huku akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza makubaliano yaliyosainiwa ili kuongeza biashara, uwekezaji na maendeleo ya pamoja kati ya mataifa hayo.
Amesema Misri ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo yenye manufaa ya pande zote, akieleza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa zaidi za kiuchumi na kuifanya Afrika kuwa na nguvu kubwa katika biashara na maendeleo ya kimataifa.









Comments
Post a Comment