VIJANA 10,000 MAFUNDI WA JIMBO LA MTUMBA WENYE UJUZI KUPATIWA VYETI VYA UFUNDI NA KUTAMBULIWA NA VETA
▪️Ni vijana wenye ujuzi lakini hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo
▪️Mbunge Mavunde aahidi kuwafikia Vijana 10,000 wenye ujuzi wa Jimbo la Mtumba
▪️Ni kupitia ya Programu ya Mama Samia ya Utambuzi wa Ujuzi chini ya VETA
▪️Mkurugenzi Mkuu VETA awataka vijana kujiunga pamoja na kuchangamkia fursa
Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde amesema kupitia Programu ya Mama Samia ya Kutambua Ujuzi wa Mafundi chini ya VETA anategemea kutambuliwa kwa zaidi ya Vijana 10,000 wenye ujuzi lakini ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo ifikapo mwaka 2030.
Mh. Mavunde ameyasema hayo jana tahere 16 Julai 2026 Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ufundi kwa vijana 100 wenye ujuzi waliotambuliwa kupitia Chuo cha VETA.
“Tunaishukuru Serikali kupitia programu hii ya Mama Samia ya kutambua ujuzi wa vijana kupitia VETA.
Vijana hawa wengi walikuwa na ujuzi lakini hawakupata nafasi ya kupata mafunzo rasmi ya ufundi kupitia vyuo vya Ufundi.
Kutambuliwa kwa ujuzi wao bila kusoma vyuo vya ufundi itakuwa ni daraja kubwa la kuwawezesha kufikia mafanikio yao ikiwemo kujiajiri wenyewe na kuajiriwa.
Ndani ya Jimbo la Mtumba tutahakikisha kila kijana mwenye ujuzi tunamtambua kwa kumpatia cheti kupitia VETA.
Tutatunza taarifa zao ili kuweza kuwasaidia kupata fursa hasa ya zabuni kupitia mpango wa PPRA wa kuzitaka Taasisi nunuzi zote za serikali kutenga 30% ya manunuzi yao ya ndani kwa ajili vya makundi ya Vijana,wakina Mama na Wenye ulemavu” Alisema Mavunde
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amesema kupitia Programu hii Vijana wenye ujuzi wa fani mbalimbali wanatembelewa na wakufunzi wa VETA katika maeneo yao na kuona shughuli mbali mbali wanazofanya kwa kuwafanyia tathmini na baadaye wakiridhishwa na uwezo ndio hutambuliwa kwa vyeti kutoka VETA.
Aidha, Kasore amewataka vijana hao kuhakikisha wanautumia vyema ujuzi walioupata ili kubadilisha maisha yao na pia kukaa kwenye vikundi vya pamoja ili iwe rahisi kuweza kupata fursa mbalimbali zinazojitokeza.












Comments
Post a Comment