Hatua za Serikali za kuendelea kuboresha maisha ya wastaafu nchini zimezaa matunda baada ya kima cha chini cha pensheni kuongezwa kutoka Shilingi 100,125.87 hadi Shilingi 250,000 kwa mwezi, ongezeko kubwa linalolenga kuongeza ustawi na kuimarisha maisha ya wanufaika wa pensheni wanaolipwa na Hazina.
Akiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma leo Juni 2, 2026, mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.), amessema Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuhakikisha wastaafu wanapata haki na stahiki zao kwa wakati.
Amesema hadi Aprili 2026, Serikali imelipa mafao ya wastaafu yenye thamani ya Shilingi bilioni 577.41, hatua inayodhihirisha uwajibikaji na utayari wa Serikali wa kuheshimu mchango wa watumishi waliolitumikia Taifa kwa miaka mingi.
Kwa upande wa hifadhi ya jamii, Serikali pia ililipa michango ya kisheria yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.428 kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama ilivyopangwa, jambo linaloimarisha uendelevu wa mifuko hiyo na kuongeza imani kwa wanachama wake.
Mhe. Balozi Omar amesema mafanikio hayo yanaakisi azma ya Serikali ya kujenga mfumo wa hifadhi ya jamii ulio imara, jumuishi na wenye kuzingatia ustawi wa wananchi, hususan wastaafu ambao wamekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa.





Comments
Post a Comment