Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, Mwita Waitara, ameibua hisia kali Bungeni baada ya kuhoji namna ambavyo baadhi ya wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma muhimu huku fedha za umma zikidaiwa kutafunwa na wachache wasiowajibika.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Fedha leo Juni 2, 2026, Jijini Dodoma, Waitara amesema ni jambo linaloumiza kuona wananchi wakihangaika kutafuta fedha za matibabu na dawa hospitalini, wakati ripoti za ukaguzi zinaendelea kuonyesha uwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma katika baadhi ya taasisi za Serikali.
Kwa sauti ya msisitizo, Waitara ameeleza kuwa fedha zinazotengwa na Bunge zinapaswa kuwafikia wananchi na kuleta maendeleo yaliyokusudiwa, badala ya kupotea mikononi mwa watu wachache wanaokwamisha juhudi za Serikali na matarajio ya wananchi.
“Leo hii kuna mwananchi anaondoka hospitalini bila dawa kwa sababu hakuna fedha za kutosha. Wakati huo huo, ripoti za ukaguzi zinaonyesha kuna watu wamechezea fedha za umma. Hili halipaswi kuvumiliwa,” amesema.
Mbunge huyo amerejea hoja zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akisisitiza kuwa hatua za kisheria na kinidhamu zinapaswa kuchukuliwa kwa haraka dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa rasilimali za Taifa.
Amesema Watanzania hawatarajii kuona hoja zilezile zikijirudia kila mwaka, bali wanataka kuona uwajibikaji, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na matokeo ya utekelezaji wa maazimio yanayotolewa na Bunge.
Waitara pia amepemdekeza kuimarishwa kwa mfumo wa ufuatiliaji wa maazimio ya Bunge ili kuhakikisha mapendekezo yanayotolewa yanageuzwa kuwa hatua za vitendo zinazolinda fedha za wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
"Fedha za umma ni jasho la wananchi. Zinapopotea, anayepoteza si Serikali pekee bali ni mwananchi wa kawaida anayekosa huduma muhimu za maisha yake."


Comments
Post a Comment