SERIKALI YAWEKA MIKAKATI MIPYA YA KUCHOCHEA UCHUMI, KULIPA MADENI NA KUIMARISHA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA
Akiwasilisha Bajeti ya wizara ya Fedha Kwa mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Jun 2,2026 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.), amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa umakini uchumi wa Taifa kwa lengo la kufikia ukuaji wa asilimia 6.3, kudhibiti mfumuko wa bei katika kiwango cha tarakimu moja na kuhakikisha akiba ya fedha za kigeni inaendelea kuwa katika viwango vinavyokidhi mahitaji ya nchi.
Katika kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, Serikali imepanga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, ugawaji wa rasilimali na usimamizi wa bajeti ili kuhakikisha fedha za wananchi zinatumika kwa tija na kuleta matokeo yanayokusudiwa.
Hatua nyingine muhimu ni kuendelea kulipa kwa wakati madeni ya Serikali, ambapo zaidi ya Shilingi trilioni 15.1 zimetengwa kwa ajili ya ulipaji wa riba na mtaji wa deni la Serikali litakaloiva, hatua inayolenga kuimarisha uaminifu wa Tanzania katika masoko ya fedha ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Serikali imetangaza kuwa itakuwa ikitoa Shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi wa umma, wakandarasi, wazabuni na watoa huduma, jambo linalotarajiwa kuongeza ukwasi katika uchumi na kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Wizara ya Fedha pia imejipanga kuboresha mfumo wa ugawaji wa rasilimali kwa kuzingatia tafiti za kitaalamu, kufanya tathmini ya Mfumo wa Bajeti unaozingatia Programu (PBB) pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) katika usimamizi wa uchumi na fedha za umma.
"Uchumi wenye nguvu haujengwi kwa bahati, bali kwa mipango madhubuti, nidhamu ya fedha na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za Taifa."
Kauli hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kujenga uchumi shindani, unaotoa fursa zaidi kwa wananchi na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya Taifa.

Comments
Post a Comment