MAPATO YA MICHEZO YA KUBAHATISHA YAFIKIA SH. BILIONI 18.76, BAHATI NASIBU YA TAIFA YAZALISHA AJIRA 484
Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya michezo ya kubahatisha nchini, hatua iliyowezesha ukusanyaji wa Shilingi bilioni 18.76 hadi Aprili 2026 pamoja na kudhibiti kwa ufanisi shughuli haramu zinazohusiana na sekta hiyo.
Akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na makadirio ya mwaka 2026/27, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania imefanikiwa kutoa leseni 7,747, kufanya kaguzi tisa za kiudhibiti na kutekeleza operesheni tatu maalumu za kukabiliana na michezo haramu ya kubahatisha.
Waziri Omar amesema mafanikio hayo yanaenda sambamba na juhudi za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kucheza kwa uwajibikaji kupitia kampeni za “Elimika na GBT”, “Mkeka Unachana” na “Wakati Wao Bado”, ambazo zimeendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, amesema Bahati Nasibu ya Taifa iliyoanzishwa Aprili 2025 imeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzalisha ajira 484, zikiwemo 29 za moja kwa moja na 455 zisizo za moja kwa moja kupitia mtandao wa mawakala.
Mbali na ajira hizo, Bahati Nasibu ya Taifa imechangia mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali, hatua inayoonesha mchango wake katika kukuza uchumi na kuongeza mapato ya umma.
"Usimamizi madhubuti wa michezo ya kubahatisha si tu unalinda maslahi ya wananchi, bali pia unafungua fursa za ajira, uwekezaji na kuongeza mapato yanayochochea maendeleo ya Taifa."





Comments
Post a Comment