MSALALA, SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuhakikisha inatekeleza kwa wakati mapendekezo yote yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akisisitiza kuwa hatua hiyo itaimarisha uwajibikaji, uwazi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Mhe. Mhita ametoa maelekezo hayo leo, Julai 8, 2026, wakati akifungua Baraza Maalumu la kujadili na kupitia hoja za ukaguzi wa CAG kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2026, lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Amesema utekelezaji wa hoja za CAG si suala la hiari, bali ni wajibu wa kila taasisi ya umma kuhakikisha dosari zilizobainishwa zinarekebishwa kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa fedha za Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Hoja za CAG zinapaswa kutazamwa kama fursa ya kuboresha utendaji wetu. Hakikisheni kila hoja inafanyiwa kazi kwa wakati na kufungwa kwa mujibu wa taratibu," amesisitiza Mhe. Mhita.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mhe. Mibako Mabubu, kwa niaba ya madiwani, amesema wamepokea maelekezo hayo na wako tayari kushirikiana kikamilifu na menejimenti ya halmashauri ili kuhakikisha hoja zote zilizobainishwa na CAG zinashughulikiwa na kufungwa kwa wakati.
Amesema ushirikiano kati ya madiwani na menejimenti utaendelea kuimarishwa ili kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha halmashauri inaendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa rasilimali zake.









Comments
Post a Comment