WANANCHI wa Mkoa wa Mara wanatarajia kupata ahueni ya huduma za afya baada ya Hospitali ya Royal Polyclinic kutangaza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuanza kutoa huduma kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hatua inayotarajiwa kupunguza usumbufu wa kusafiri nje ya mkoa kutafuta matibabu ya kibingwa.
Akizungumza katika Hospital ya Royal Polyclinic Musoma, Mkurugenzi wa Royal Polyclinic, Stella Eyembe, amesema hospitali hiyo imekamilisha taratibu muhimu za kuingia mkataba na NHIF na muda si mrefu wanachama wa mfuko huo wataanza kupata huduma zote za matibabu katika hospitali hiyo.
"Kwa muda mrefu wananchi wengi wa Mkoa wa Mara walitamani huduma za NHIF zipatikane Royal Polyclinic. Sasa tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba, na hivi karibuni wanachama wa NHIF wataanza kuhudumiwa hapa kwa urahisi na kwa viwango vya juu," amesema.
Ameongeza kuwa mbali na NHIF, hospitali hiyo tayari inapokea wagonjwa kupitia bima nyingine mbalimbali huku ikiendelea kupanua ushirikiano na mifuko mingine ya bima ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bila kikwazo cha gharama.
Stella amesema Royal Polyclinic ilianzishwa Julai mwaka 2020 chini ya kampuni ya IKCS Medical Company Limited, ikiwa na dhamira ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Amesema uwekezaji huo ulitokana na maamuzi ya Dkt. Eyembe, mzaliwa wa Mkoa wa Mara, aliyerejea nyumbani kuwekeza katika sekta ya afya ili kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa zilizokuwa zikipatikana kwa shida.
"Tuliona wananchi wengi walikuwa wakisafiri kwenda Mwanza na maeneo mengine kupata huduma za kibingwa. Tukasema huduma hizo ziletwe Mara ili ziwafikie wananchi kwa gharama nafuu na kwa wakati," amesema.
Kwa mujibu wa Stella, Royal Polyclinic kwa sasa inatoa huduma za madaktari bingwa, maabara yenye vifaa vya kisasa, ultrasound, fiziotherapia, huduma za meno, dawa na huduma nyingine za uchunguzi na matibabu.
Amesema hospitali hiyo itaendelea kuwekeza katika vifaa vya kisasa na kuongeza huduma ambazo bado hazipatikani kwa urahisi mkoani Mara ili kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za nje ya mkoa.
Akizungumzia mipango ya baadaye, Stella amesema hospitali hiyo inalenga kukua na kuwa Hospitali ya Kanda (Zonal Hospital) pamoja na kufungua matawi katika wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, akisema ushirikiano wanaoupata kutoka ngazi ya wilaya, mkoa na taifa umeiwezesha Royal Polyclinic kupanua huduma zake kwa kasi.
"Serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji. Tunaendelea kupata ushirikiano mkubwa na ndiyo maana tuna uwezo wa kupanua huduma zetu. Dhamira yetu ni kuhakikisha kila mwananchi wa Mara anapata huduma za afya za kisasa karibu na alipo," amesema.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Afya ya Kinywa na Meno wa Royal Polyclinic, Dkt. Immanuel Sanga, amesema magonjwa ya kinywa na meno ni changamoto kubwa mkoani Mara, hasa kwa wachimbaji madini na wavuvi ambao mara nyingi hushindwa kuzingatia usafi wa meno kutokana na mazingira ya kazi.
Amesema sababu kuu za magonjwa hayo ni kutofanya usafi wa kinywa na meno pamoja na ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi.
Amewashauri wananchi kusafisha meno kila baada ya kula, kupunguza vyakula vinavyoshikamana kwenye meno na kufuata utaratibu wa kula milo mitatu kwa siku ili kulinda afya ya kinywa na meno.








Comments
Post a Comment