Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari, amewataka Mawakili wa Serikali nchini kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha utawala wa sheria, kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na kutoa ushauri wa kisheria wenye tija ili kuiwezesha Tanzania kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Johari alitoa kauli hiyo Julai 15, 2026, alipofungua rasmi msimu wa tatu wa Mafunzo ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali yanayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), yatakayodumu hadi Julai 17, 2026.
Amesema mafanikio ya Dira ya Taifa 2050 hayatapatikana kwa uwekezaji pekee, bali yanahitaji mifumo imara ya sheria, sera zenye mwelekeo sahihi, taasisi zenye uwezo na wataalamu wa sheria watakaoisimamia Serikali kwa weledi na uadilifu.
"Nitumie fursa hii kuwakumbusha washiriki wote kuwa, tunapoendelea kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 ni muhimu kufahamu kuwa Taifa linahitaji zaidi ya utaalamu wetu wa sheria," amesema Johari.
Ameeleza kuwa Mawakili wa Serikali wanabeba jukumu kubwa la kuhakikisha sheria, sera na mikataba yote ya Serikali inalinda maslahi ya Taifa na kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayoendelea duniani.
Johari amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kujijengea uwezo wa kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuibua suluhisho za changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumzia maendeleo ya teknolojia, amesema mageuzi ya kidijitali yamebadili kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za kisheria, hivyo Mawakili wa Serikali wanapaswa kuyamudu matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) pamoja na ushahidi wa kielektroniki ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.
"Mapinduzi ya teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa namna ambavyo huduma za kisheria zinaendelea kutolewa nchini na duniani kote. Hivyo, Mawakili wa Serikali hawawezi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kutumia mazoea ya zamani," amesisitiza.
Aidha, amewahimiza kuendelea kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji, uzalendo na nidhamu, akieleza kuwa wananchi wanatarajia kuona sheria zikitumika kulinda rasilimali za umma na kuwa msingi wa maendeleo ya Taifa.
"Wananchi wanatarajia kuona rasilimali za umma zikilindwa kwa wivu mkubwa na sheria zikitumika kama nyenzo muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050," amesema.
Kwa upande wake, Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Prof. Florens Luoga, akiwasilisha mada kuhusu "Nafasi ya Kimkakati ya Mawakili wa Serikali katika kufikia Dira ya Taifa 2050," amesema Mawakili wa Serikali ni nguzo muhimu katika kuharakisha mageuzi ya kiuchumi kupitia ushauri bora wa kisheria.
"Wakili wa Serikali ana nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi na kulinda maslahi ya Taifa, kwa kuwa ushauri wa kisheria anaoutoa ni kichocheo muhimu cha mageuzi ya kiuchumi," amesema Prof. Luoga.
Awali, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole, alimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuwezesha mafunzo hayo, akisema yataongeza uwezo wa Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Sheria, Bi. Neema Ringo, alisema mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajengea washiriki uwezo wa kitaaluma kupitia mada zitakazowasilishwa na wakufunzi wabobezi wa ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ya Bespoke yanawakutanisha Mawakili wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha ujuzi wao katika masuala ya sheria, uchumi na utawala bora, sambamba na kuandaa wataalamu watakaosaidia kuifikisha Tanzania kwenye malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.










Comments
Post a Comment