📌*Umeme sasa ni Kitongoji kwa Kitongoji*
📌*Nishati safi ya Kupikia kwa kila mwananchi*
📍*Arusha*
Wananchi wa Wilaya ya Arumeru Mashariki mkoani Arusha wameendelea kupata elimu kuhusu huduma za umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia ziara ya uhamasishaji iliyofanywa na maafisa wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Elimu hiyo ilitolewa leo wakati maafisa wa REA walipotembelea baadhi ya vijiji na vitongoji vinavyotekelezwa miradi mbalimbali ya nishati, ikiwemo miradi ya usambazaji wa umeme katika vitongoji pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama vile gesi na majiko banifu.
Katika ziara hiyo, wananchi walipatiwa elimu kuhusu taratibu za kufanya maombi ya kuunganishiwa umeme, gharama za uunganishaji wa huduma hiyo pamoja na tahadhari ya kujiepusha na matapeli maarufu kama vishoka, ambao huwalaghai wananchi kwa kuwatoza fedha kinyume na utaratibu rasmi.
Aidha, wananchi walihimizwa kujiunga na huduma ya umeme wakati mkandarasi bado yupo katika eneo la mradi, kwani hatua hiyo hurahisisha upatikanaji wa huduma kwa gharama nafuu. Walielezwa kuwa Serikali tayari imegharamia ujenzi wa miundombinu ya kufikisha umeme katika maeneo yao, hivyo mwananchi anabaki na jukumu la kuweka mfumo wa waya (wiring) ndani ya nyumba na kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ya shilingi 27,000 tu.
Maafisa wa REA pia waliwahimiza wananchi kutumia umeme kwa shughuli za uzalishaji mali ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao. Walisisitiza kuwa dhana ya “Kijijini kama Mjini” inapaswa kutekelezwa kwa vitendo kupitia matumizi ya umeme katika biashara, viwanda vidogo, huduma za kijamii na shughuli nyingine za maendeleo, badala ya kubaki kuwa nadharia.
Vilevile, wananchi walikumbushwa umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme kwa kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi hiyo. Walihimizwa kushiriki kulinda miundombinu hiyo na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona vitendo vinavyoweza kuhatarisha au kuharibu huduma ya umeme.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za REA za kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu huduma za umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kuongeza matumizi ya nishati hizo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo ya vijijini.


Comments
Post a Comment