NA MASHAKA MHANDO, Tanga
SERIKALI imetoa ahadi ya kutoa Shilingi milioni 750 ili kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyosalia katika Kituo kipya cha Afya cha Maweni, jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Tanga ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kituo cha afya Maweni sambamba na mradi wa mabweni katika shule ya sekondari Usagara na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Balozi Omar alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali imejitahidi kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wa Tanga kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Kwa mwaka huu wa fedha uliopita, Mkoa wa Tanga ulipangiwa kutumia Shilingi bilioni 528.1, na Serikali imewasilisha kiasi cha bilioni 487.5. Hii ni zaidi ya asilimia 92 ya fedha zote za maendeleo zilizopangwa," alisisitiza Balozi Omar.
Katika hali ya kuonyesha kuridhishwa na usimamizi wa fedha za umma, Waziri huyo aliipongeza uongozi wa Bandari ya Tanga kwa utendaji uliovuka malengo.
"Serikali iliwekeza Shilingi bilioni 429.1 katika Bandari ya Tanga, na hadi sasa bandari hiyo imeingiza mapato ya shilingi bilioni 436. Kiukweli mmekusanya vizuri; fedha zimerudi na chenji imebaki juu," alisema Waziri kwa msisitizo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, Meja (Mst) Hamis Mkoba aliiomba serikali kuwasaidia kupata kiasi cha Shilingi bilioni 24.7 ambazo zinatokana na kodi ya mapato zimekwama katika baadhi ya taasisi tangu mwaka 2022. Alisema fedha hizo zingekuwa msaada mkubwa katika kuongeza kasi ya maendeleo ya jiji hilo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Jiji (DMO), Dkt. Stephen Mwandambo alieleza kuwa kituo hicho cha Maweni ni mkombozi kwa wananchi 40,740 wa kata hiyo, ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za uzazi na matibabu.
Aidha, Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga shilingi milioni 75 kwa ajili ya mwaka wa fedha ujao ili kukamilisha ujenzi wa baadhi ya majengo yaliyobaki, ikiwemo kichomea taka, ukamilishaji wa jengo la upasuaji, na wodi ya wazazi, ili kuimarisha huduma katika kituo hicho.
Pamoja na utekelezaji huo, bado kuna majengo nane yanayohitajika kujengwa ili kukamilisha kituo hicho kuwa kituo cha afya kamili, ikiwemo jengo la utawala, jengo la kulelea watoto (mama na mtoto), wodi za kulaza wagonjwa, jengo la x-ray, nyumba za watumishi, jengo la kuhifadhia maiti, njia za kupitishia wagonjwa (walkway), na wigo wa usalama.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Tanga Dadi Kolimba alisema kuwa serikali katika mwaka wa fedha 2025/26 waliweza kuleta kiasi cha sh Shilingi bilioni 357 kwa miradi ya maendeleo ya Jiji.
Alisema kuwa miongoni mwa fedha hizo takribani sh bilioni 1.8 zimetengwa, kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika sekta ya afya huku hospitali ya wilaya ya Masiwani ikipata bilioni 2.9.
"Aidha Shilingi milioni 548 zimetumika kwa nyumba za watumishi, kituo cha Mleni,Maweni ,Pande na Chongoleani.
Juma abdala mkazi wa kata ya Maweni amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kuwahakikishia huduma za afya na kutokwenda umbali mrefu wakifuata huduma hiyo.
"Ujenzi wa Kituo hiki umekuwa na mchango mkubwa sana wa huduma za afya ,serikali ikitekeleza ahadi yake hiyo huduma zitaongezeka na kuboreka zaidi,"anasema.



Comments
Post a Comment