SERIKALI imeagiza kuimarishwa mara moja kwa doria na msako mkali dhidi ya biashara haramu ya magendo katika mpaka wa Horohoro, uliopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, ikiwa ni hatua madhubuti ya kudhibiti uvujaji wa mapato na kulinda usalama wa Taifa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alipofanya ziara ya kimkakati katika Kituo cha Forodha cha Horohoro kujionea shughuli za ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa biashara ya kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
Balozi Omar aliweka wazi kuwa udhibiti wa magendo sio tu suala la kuongeza mapato ya Serikali, bali ni msingi mkuu wa kulinda usalama wa nchi na kuhakikisha Taifa linakuwa na takwimu sahihi za kiuchumi.
Jukumu Sio Kukusanya Mapato Tu
Waziri huyo aliwapongeza maofisa wa forodha kwa kazi wanayofanya, lakini aliwataka kuongeza umakini maradufu kudhibiti bidhaa zilizopigwa marufuku kuingia nchini na zile zinazokwepa kufuata masharti ya kisheria.
"Tusipotekeleza jukumu hili ipasavyo tunaweza kulisababishia Taifa madhara makubwa. Sisi maofisa wa forodha hatuna jukumu la kukusanya mapato pekee, bali pia kuhakikisha bidhaa zilizopigwa marufuku haziingii nchini. Usalama wa Taifa ni jambo ambalo hatuwezi kulifumbia macho," alionya Balozi Omar.
Aliongeza kuwa Serikali inahitaji takwimu sahihi za biashara ili kupanga mipango ya maendeleo, jambo ambalo haliwezekani kama magendo yataachwa yashamiri mipakani. Aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyombo vya ulinzi, na Kamati za Usalama kushirikiana kikamilifu kumaliza tatizo hilo.
Changamoto ya 'Scanner' na Umeme
Akiwasilisha taarifa ya utendaji mbele ya Waziri, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Horohoro, Shadrack Mbonea, alibainisha baadhi ya vikwazo vinavyochelewesha ufanisi, ikiwemo ukosefu wa mashine ya kisasa ya kukagua mizigo (Scanner).
Mbonea alieleza kuwa ununuzi wa mashine hiyo tayari upo kwenye mpango wa utekelezaji wa Serikali kwa miaka ya fedha 2026/2027 na 2027/2028.
Vilevile, aliiomba Serikali kukipatia kituo hicho njia maalumu ya umeme wa uhakika (Dedicated Line), kwani kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na uchakavu wa miundombinu, jambo linalokwamisha utoaji wa huduma kwenye lango hilo muhimu.
'Njia za Panya' na Barabara ya Mpakani
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, aliibua hoja ya ukosefu wa miundombinu bora ya barabara za mpakani, akieleza kuwa inatoa mwanya kwa wahalifu kutumia njia zisizo rasmi (njia za panya) kuingiza magendo kutoka Kenya.
"Ujenzi wa barabara ya mpakani ni ahadi iliyotolewa na Serikali. Tunaomba ujenzi wa barabara hiyo uharakishwe kwa kuwa utasaidia kudhibiti njia hizi zisizo rasmi zinazotumiwa na wafanyabiashara wa magendo, na hivyo kuimarisha ulinzi na usalama wetu hapa mpakani," alisisitiza Mhe. Kalima.




Comments
Post a Comment