CHATANDA: MAMA TIBAIJUKA, TUJENGE MSINGI WA UTII WA SHERIA NA SI MASHINIKIZO YA KUFUTA KESI KWA JINA LA MARIDHIANO
NA: MWANDISHI WETU
Mwenyekiti Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amemshauri aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, kuwa balozi wa kuhimiza viongozi na wananchi kutii sheria za nchi ili kuepuka kuingia katika mikono ya vyombo vya sheria.
Chatanda ameyasema hayo Julai 14, 2026, kufuatia ujumbe alioandika Prof. Tibaijuka katika Mtandao X, kuhusiana na kesi inayomkabili Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Katika ujumbe wake, Prof. Tibaijuka amesema "Dkt. Samia Suluhu, Mhe. Rais naendelea kushauri kwa dhati Tundu Lissu aachiwe huru kwani kesi haikamiliki, hekima na busara iliyotufanya kuitangaza sera ya 4Rs ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili".
"Simulizi hizi za kutisha za vyombo vya habari vya kimataifa zinainua hisia kali hasa kwa vijana, hata wazee tumekumbushwa kadhia ya operation Sogeza na iliyounda Vijiji vya Ujamaa 1974-1976, taarifa hizi zinaathiri kikubwa taswira ya Taifa letu na maslahi yake, athari ni kubwa".
"Tutafute muafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano, tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake mfano wa risasi 16 kushindwa kukomesha uhai ingawa maumivu ni makubwa, tutubu na kusali kuliombea Taifa letu kila mtu kwa imani yake," ameongeza Prof. Tibaijuka katika andiko lake hilo.
Kutokana na andiko hilo, Chatanda amesema nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na ni vyema mahakama iachwe ifanye kazi yake ili haki itendeke.
"Tusiruhusu utamaduni wa jambo linapokuwa mahakama, basi tuanze kumshinikiza Rais aingilie kati na kulimaliza. Tuiache mahakama ifanye kazi yake, na pale itakapothibitika kuwa mtuhumiwa hana hatia, basi ataachiwa huru," amesema Chatanda.
Sambamba na hilo, amesema, Tanzania ni nchi huru yenye mamlaka kamili na inaendesha mambo yake kwa mujibu taratibu zilizopo, hivyo hata vyombo vya habari vya kimataifa vinapaswa kuheshimu taratibu zetu za uendeshaji wa nchi na mashauri ya kisheria.
"Tusiruhusu kila kinachoandikwa katika vyombo vya habari vya kimataifa kikayumbisha na kusababisha kuacha kusimamia sheria za nchi, ni lazima tuheshimiane linapokuja suala la utii wa sheria za nchi," amesema.
Sanjari na hilo, Chatanda amesema, mataifa yaliyoendelea ni watii wazuri wa sheria zao, hivyo na sisi Watanzania tuwe na utamaduni wa kuheshimu sheria na mamlaka zilizopo na kutambua kuwa kamwe maridhiano si mbadala wa uvunjifu wa sheria.
"Dhana ya maridhiano isitumike vibaya, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa maridhiano na hata alivyoingia madarakani aliwarejesha viongozi wa upinzani waliokuwa nje ya nchi, akawakaribisha warudi nyumbani ili nao watoe mchango wao katika ujenzi wa taifa, lakini baadhi yao ndo wamekuwa vinara wa kutoa kauli za kebehi na dharau kwa viongozi na serikali, hivyo tunapohimiza maridhiano, tusisahau pia utii wa sheria," amesema.
Katika hatua nyingine, Chatanda ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuheshimu sheria za nchi ili kuepuka mkono wa sheria kwani nchi yetu inaongozwa kwa kuzingatia utawala wa sheria. Pia, amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda amani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Comments
Post a Comment