WAZIRI MAVUNDE ATOA WITO WAMILIKI WOTE WA LESENI ZA UCHIMBAJI WA MADINI KINYWE KUANZA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MARA MOJA
■ Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa madini kinywe ifikapo Mwaka 2030
■ Serikali yasaini mkataba wa ubia na Kampuni za Grafica na Eminent.
■ Aitaka Timu ya majadiliano ya serikali kuanza mchakato wa majadiliano na Wamiliki wa Leseni 27
■ Amshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha sekta ya madini,
■ Ruangwa kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani na teknolojia ya madini kinywe duniani.
*Ruangwa, Lindi*
Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* ameielekeza Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye Sekta ya Madini (GNT) kuwaita na kufanya nao majadiliano wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kinywe nchini Tanzania kujadiliana kuhusu ubia wa serikali katika Kampuni hizo na kuwataka kuanza utekelezaji wa uchimbaji kwa mujibu wa masharti ya leseni na Sheria ya Madini Sura ya 123.
Ameyasema hayo leo tarehe 30 Mei, 2026 Wilayani Ruangwa aliposhiriki zoezi la utiaji saini na Kampuni za Grafica Resources na Eminent Minerals Limited zenye ubia wa uwekezaji wa hisa asilimia 83 na Serikali asilimia 17 kwa kila kampuni.
"Sisi sekta ya madini tunamshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotupa maelekezo na kutuwezesha kusimamia sekta kikamilifu kwa maendeleo ya Taifa letu"
"Na ndiyo maana Kampuni zote ambazo hazijaanza uzalishaji kwa mujibu wa masharti ya leseni zao tumeziandikia hati ya makosa (Default Notice) kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123. Kusaini kwetu mikataba siku ya leo, hakutoi unafuu kwa wawekezaji hawa kutotekeleza uwekezaji wao kwa mujibu wa Sheria yetu ya madini" amesisitiza Mhe. Mavunde.
Waziri Mavunde amesema hatua ya Timu ya GNT kuwaita na kuwataka wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kinywe kufuata masharti ya Sheria na kuanza uzalishaji kutapelekea ufikiaji wa lengo la kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa kwanza duniani wa madini kinywe ifikapo mwaka 2030.
Vilevile, Waziri Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wa miradi hiyo kutoa fursa ya kipaumbele cha ajira kwa watanzania hususan wanaozunguka miradi hiyo. Kwa kufanya hivyo kutachochea uchumi wa Vijiji, Wilaya ya Ruangwa hususan kupitia wajibu wa uwekezaji kwa jamii (CSR) na kupelekea maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.
Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa miradi hiyo itakapoanza kuzalisha kikamilifu, itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 101,048 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Grafica na tani 15,930 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Eminent mtawalia, hali inayoifanya Ruangwa sasa kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani wa teknolojia za kisasa duniani.
Waziri Mavunde pia ameeleza kuwa bado Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika uzalishaji wa madini mbalimbali duniani, na ndiyo maana tunaendelea kuweka mkazo kwenye ufanyaji wa utafiti wa kina ili kubaini mashapo zaidi yatakayoongeza uchimbaji hususan kupitia wachimbaji wadogo wenye mchango mkubwa katika uchumi wetu.
Awali, akieleza mchakato wa kufikia makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye sekta ya Madini, *Prof. Sifuni Mchome* amebainisha kuwa, majadiliano hayo yalifanyika kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi yetu na hayakuwa na lengo la kutafuta mshindi, hali iliyopelekea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hisa zisizofifishwa za asilimia 17 kwenye kila mradi wa ubia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Grafica Resources, *Bw. Vikas Bardiya* ameeleza kuwa kampuni yao inaishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyowapa mpaka kufikia makubaliano ya kuwekeza na kuahidi kwamba watahakikisha wanatekeleza uwekezaji huo kwa mujibu wa mkataba ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi wa Ruangwa na Taifa kwa ujumla.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Eminent Minerals Limited, *Bw. Shafiqali Khaki* ameeleza kufarijika kwao kuwa kampuni ya kizawa kuingia ubia na Serikali katika uwekezaji kwenye mradi huo wa uchimbaji madini kinywe na kwamba wao kama wazawa watahakikisha sehemu kubwa ya zaidi ya ajira 250 zitakazozalishwa katika uwekezaji huo zinachukuliwa na watanzania ili kuinua uchumi wa Taifa letu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, *Mheshimiwa Zainab Telack* alimshukuru Mhe. Rais kwa kuwa kiongozi mahiri katika kusimamia uchumi na kuhakikisha rasilimali zetu zinanufaisha watanzania. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Lindi itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ili waweze kuendesha shughuli zao kwa kasi na kunufaisha wananchi wa Lindi na Taifa kwa ujumla.






Comments
Post a Comment