Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Simeone Nyansaho, ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Mkuu wa Majeshi kuendelea kutoa kipaumbele kwa michezo inayokuza na kuibua vipaji vinavyoweza kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, hususan mchezo wa riadha na michezo mingine ya ushindani.
Akizungumza Julai 13, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2026), Dkt. Nyansaho amesema kaulimbiu ya mashindano hayo isemayo "Umoja, Amani na Mshikamano kwa Ujenzi wa Taifa Letu Imara" inalenga kuimarisha mshikamano miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.
Aidha, Waziri Nyansaho amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, kwa maandalizi ya mashindano hayo na ushiriki wa kamandi mbalimbali za JWTZ, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uadilifu, haki na ushindani wa kweli ili kupata washindi wanaostahili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, amesema ana imani mashindano hayo yataendelea kuwa chachu ya kuibua wanamichezo wenye uwezo mkubwa wa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa na kuongeza idadi ya medali za dhahabu kupitia michezo mbalimbali.
Jenerali Mkunda amesema CDF Cup 2026 pia inalenga kuimarisha timu za michezo za JWTZ, kukuza nidhamu kwa wanamichezo pamoja na kuhakikisha sheria na kanuni za kila mchezo zinazingatiwa wakati wote wa mashindano.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2026), Brigedia Jenerali Said Hamis Said, amesema mashindano hayo yameanza rasmi leo na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 29, 2026, yakihusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, kuogelea, mishale, ngumi na soka la ufukweni.
Brigedia Jenerali Said amesema pamoja na kuibua vipaji vya wanamichezo, mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya ushiriki wa JWTZ katika mashindano ya kitaifa na kimataifa. Aidha, amewakaribisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, akibainisha kuwa viingilio ni bure.
Ufunguzi wa CDF Cup 2026 uliambatana na shamrashamra mbalimbali zikiwemo gwaride la heshima, maandamano ya timu shiriki na burudani zilizodhihirisha umoja, nidhamu na uzalendo wa wanajeshi pamoja na washiriki wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanajeshi kutoka kamandi mbalimbali, huku yakitoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kukuza ushindani wenye tija na kuendeleza utamaduni wa michezo ndani ya JWTZ.
Kwa kuanza rasmi kwa CDF Cup 2026, matarajio ni kuona ushindani wa hali ya juu utakaoibua vipaji vipya na kuimarisha uwezo wa wanamichezo wa JWTZ, hatua itakayochangia kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano ya kikanda na kimataifa.









Comments
Post a Comment