MBUNGE wa Jimbo la Tarime Mjini, Mhe. Esther Matiko, amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na ndoto kubwa maishani, huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio yao ya baadaye.
Akizungumza na wanafunzi wakati wa ziara yake katika shule mbalimbali za jimbo hilo, ikiwemo shule ya Msingi Nyamisangura, Magufuli, shule ya msingi Tarime, Mhe. Matiko amesema awali alifika kuzungumza na walimu na kukabidhi saruji kwa ajili ya kuboresha sakafu za madarasa, lakini alipokutana na wanafunzi aliamua kuwasalimia na kuzungumza nao.
"Nimefurahi sana kuwaona na kuwasalimia.Nawapenda sana. Leo nimetembelea shule tano na katika shule zote mmeonyesha nidhamu na ari kubwa ya kujifunza," amesema.
Kutokana na kufurahishwa na mapokezi aliyoyapata, Matiko alitangaza kutoa gunia 16 za mahindi kwa shule mbalimbali ili kuunga mkono mpango wa chakula shuleni, akieleza kuwa lishe bora itawasaidia wanafunzi kujifunza kwa umakini na kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
Pia aliwahimiza wazazi kuendelea kuchangia mpango wa chakula shuleni ili kuhakikisha watoto wanapata chakula cha kutosha wanapokuwa shuleni.
Kwa upande wa wanafunzi, aliwataka kutumia fursa ya elimu kwa juhudi na nidhamu, akisema wanapaswa kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao za kuwa madaktari, walimu, wahandisi na wataalamu wa fani mbalimbali.
"Wangapi mnataka kufanya vizuri kwenye masomo? Wangapi mnataka kufikia ndoto zenu? Basi someni kwa bidii na msikate tamaa," aliwaambia wanafunzi.
Sambamba na hayo amewataka wanafunzi hao kufikisha salamu zake Kwa wazazi wao huku akiwahimiza wawaambie wazazi wao wamuunge mkono ili kutimiza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekata ya Elimu nchini.
Aidha, aliipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya shule na sekta ya elimu nchini, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na walimu, wazazi na wananchi katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa manufaa ya wanafunzi wa Jimbo la Tarime Mjini.


Comments
Post a Comment