Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha waathirika wanapata huduma za tiba na marekebisho ya tabia.
Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Mei 29,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2025.
Amesema katika mwaka huo, jumla ya watu 85,425 wenye uraibu wa dawa za kulevya walipatiwa huduma za tiba kupitia vitengo vya afya ya akili vilivyopo katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda, kliniki za MAT pamoja na nyumba za upataji nafuu nchini.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha waathirika wanapata huduma stahiki zinazowasaidia kurejea katika maisha ya kawaida na kuwa sehemu ya kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, Profesa Kabudi amesema Serikali pia imeendelea kuimarisha elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji zinazofanyika katika jamii, taasisi za elimu pamoja na vyombo vya habari.
Amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wananchi, kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, na kuwalinda dhidi ya matumizi pamoja na biashara ya dawa za kulevya.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ili kulinda afya ya wananchi, usalama wa jamii na nguvu kazi ya taifa




Comments
Post a Comment