SERIKALI YASISITIZA KUHARAKISHWA UJENZI WA OFISI ZA MIKOA ILI KUONGEZA NGUVU ZA UDHIBITI DAWA ZA KULEVYA
SERIKALI imesisitiza kuharakishwa kwa ujenzi na uanzishwaji wa ofisi za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika mikoa yote inayotajwa kuwa njia kuu za mapito ya dawa za kulevya, ili kuongeza kasi ya udhibiti na kuimarisha mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.
Akizungumza leo Mei 29,2026 Jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Palamagamba Kabudi amesema ni muhimu kuharakisha ujenzi na uanzishwaji wa ofisi katika mikoa yote inayotumika kama njia za mapito ya dawa za kulevya ili kuongeza ufanisi wa udhibiti na operesheni.
Amesema kuwa ujenzi wa ofisi hizo lazima uendane na kuimarishwa kwa uwezo wa kiutendaji wa mamlaka hiyo.
“Tumeamua pia kuimarisha uwezo wa kiutendaji ikiwemo kununua magari 17 yatakayosaidia kuongeza nguvu za operesheni za udhibiti, ufuatiliaji na ukamataji wa mitandao ya dawa za kulevya,” amesema.
Prof. Kabudi amesema Katika kuimarisha mapambano hayo, Serikali imeendeleza ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia na kufanya operesheni za pamoja.
Serikali imeeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanatokana na dhamira thabiti ya uongozi wa nchi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama, wataalamu wa afya, wadau na wananchi.
Aidha, Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazotoa matibabu ya uraibu wa dawa za kulevya bure.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazotoa matibabu ya uraibu wa dawa za kulevya bure, na hatua hii imeokoa maisha ya watu wengi,” amesema
Kutokana na mafanikio hayo, Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa kama mfano bora katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema pia Serikali itaendelea kuimarisha ofisi za mamlaka hiyo katika mikoa mbalimbali, sambamba na kuongeza kasi ya operesheni dhidi ya mirungi, bangi na dawa mpya zinazojitokeza.
Sambamba na hayo,Prof. Kabudi amesema Serikali imeweka mkazo katika utafiti kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu ili kuboresha mbinu za udhibiti na tiba.
“Utafiti ni muhimu ili kuendana na mabadiliko ya mbinu zinazotumiwa na mitandao ya dawa za kulevya,” ilisisitizwa.
Pia, kupitia ushirikiano na VETA, waraibu waliopata matibabu wanapatiwa mafunzo ya stadi za kazi ili kuwawezesha kujitegemea baada ya urejeo katika jamii.
Amesema sema pia serikali imedhamiria kuwekeza katika teknolojia za kisasa ikiwemo akili unde (Artificial Intelligence) ili kuimarisha utambuzi na udhibiti wa dawa za kulevya nchini.


Comments
Post a Comment