Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo amesema serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro ya Ardhi nchini, hatua inayolenga kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri wananchi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumza leo Mei 28 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Dkt. Leonard Akwilapo amesema mkakati huo umeandaliwa kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu na kuhakikisha matumizi ya ardhi yanafanyika kwa utulivu, haki na maendeleo endelevu.
Amesema hatua hiyo inatekelezwa kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba aliyeitaka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa mpango maalumu wa kushughulikia chanzo cha migogoro hiyo nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, mkakati huo umehusisha makundi yote muhimu yanayotumia ardhi ikiwemo wakulima, wafugaji, wawekezaji pamoja na mamlaka za hifadhi, kwa lengo la kujenga mfumo utakaosaidia kuzuia migogoro kabla haijawa mikubwa na kuhakikisha kila upande unapata haki yake.
Amesema serikali inaamini kuwa kudhibiti migogoro ya ardhi kutasaidia kuongeza amani na utulivu katika jamii, kuimarisha shughuli za uzalishaji na uwekezaji pamoja na kuwapa wananchi mazingira bora ya kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa uhakika zaidi.
Aidha, Dkt. Akwilapo amempongeza Waziri Mkuu kwa dhamira yake ya kutafuta suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi, akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza tija katika matumizi ya ardhi na kuchochea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


Comments
Post a Comment