Na Angela Sebastian ;Kagera
Mahakama ya Wilaya ya Karagwe imemtia hatiani Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chagati, Robson Andrea Nganshinga, kwa kosa la rushwa baada ya kubainika kuwa alitoa barua ya utambulisho iliyomwonyesha mtu aliyedaiwa kuwa raia wa Burundi kuwa ni Mtanzania ili apate ajira katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (KDCU).
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi (SRM), Charles Ngonyani, katika shauri la rushwa namba 15343/2026.
Akizungumza leo mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Ismail Bukuku, amesema mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, Toleo la Mwaka 2023.
Bukuku alisema uchunguzi ulionyesha kuwa Nganshinga aliidhinisha barua ya kumtambua Fabuan John, anayefahamika pia kwa jina la Dusabimana Fabiice, kuwa ni mkazi na raia wa Tanzania, huku akijua kuwa alikuwa raia wa Burundi.
Amesema lengo la barua hiyo lilikuwa kumwezesha mtu huyo kupata ajira katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (KDCU), jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi, mahakama ilimkuta mshtakiwa na hatia na kumhukumu kulipa faini ya Shl. 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Mshtakiwa alichagua kulipa faini hiyo, ambapo shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Mohamed Kassim Mtambo.
Hukumu hiyo ni sehemu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa na TAKUKURU katika kuwawajibisha watumishi na viongozi wanaokiuka sheria za kupambana na rushwa, hususan katika utoaji wa nyaraka zinazoweza kutumika kupata huduma au fursa kwa njia zisizo halali.






Comments
Post a Comment